Wednesday, February 13, 2013

KWARESIMA

“Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza. Rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie  Bwana…” (Yoe 2:12)

Leo Kanisa limeanza kipindi cha Kwaresima. Hizi ni siku arobaini za sala, mafungo, kujinyima, kutubu na kuwasaidia wahitaji. Ni kipindi cha maandalizi ya sikukuu ya Ufufuko wa Yesu. Neno linalotuongoza ni wongofu. Kwaresima ni safari inayomrudisha mkristo kwenye njia ya wongofu: nirudieni mimi! Hivyo ndivyo Bwana anavyotuhimiza. Anataka tumrudie, si kwa matendo ya nje, bali kwa mioyo yetu yote kwa kurarua mioyo na si mavazi.


Mafungo ya Kwaresima si ya kujikatalia kula tu, bali pia kuacha kabisa mawazo, maneno na matendo yanayopunguza mwendo wetu wa safari ya kiroho. Ni kipindi cha ibada ya moyo na cha kutenda matendo ya huruma yanayoonesha mshikamano wa kibinadamu na upendo wa kikristo unaookoa. Kama anavyosema Mt. Petro Krisologo; “Matendo ya huruma na ibada ndiyo mabawa ya mfungo… mfungo bila matendo ya huruma ni sanamu ya njaa, ni muonekano wa nje usio na thamani ya utakatifu. Bila ibada mfungo ni fursa ya ubinafsi… tunapofunga, ndugu zangu, tuweke chakula chetu mikononi mwa maskini” (Petro Krisologo, Omelia VIII, Sul digiuno della Quinquagesima)

Kipindi hiki kinapaswa kuwa kipindi kinachotusaidia kuanza tukio la kinabii, tukio linalosaidia kuyabadili maisha yetu na ya wenzetu. Katika Biblia Musa anafunga siku arobaini usiku na mchana kabla ya kupokea Amri Kumi za Mungu (Rej. Kut 34:28), anafanya hivyo pia Elia kabla hajakutana na Mungu juu yam lima Horebu (1Fal 19:8), hali kadhalika Yesu kabla hajaanza utume wake.

Majivu na maji


Kipindi cha Kwaresima kinaanza siku ya Jumatano ya Majivu. Don Tonino Bello, aliyekuwa Askofu wa Molfetta, Italia anaandika kuwa safari yote ya mkristo ni kuanzia kichwani hadi miguuni. Ni safari inayoelezwa vizuri kwa ishara ya majivu tunayopakwa kichwani na maji anayotumia Yesu kuwaosha mitume wake miguu. Ni safari inayoanzia kwenye toba na kuishia kwenye utumishi. “Toba na utumishi”, anasema Don Tonino Bello, “ni mahubiri makuu ambayo kanisa linayakabidhi kwa majivu na maji, kuliko kwa maneno”. Kwa maneno mengine ndiyo kusema kuwa mahubiri yetu hayawezi kuielezea vizuri zaidi safari ya uongofu kama jinsi ambavyo ishara ya majivu na maji inavyoweza kufanya. Tumrudie Mungu kwa moyo wa toba na katika utumishi tuzidi kuiona ile sura ya Mungu katika mahujaji wote walio katika safari ya maisha. 



Tuesday, February 12, 2013

BENEDIKTO XVI ATANGAZA KUACHILIA MADARAKA YA KULIONGOZA KANISA

Baba Mtakatifu Benedikto XVI ametangaza azma yake ya kuachilia madaraka ya kuliongoza Kanisa Katoliki ifikapo tarehe 28 Februari 2013. Habari hii imepokelewa kwa hisia tofauti na kwa mshtuko mkubwa. Kulingana na taratibu za Kanisa, Baba Mtakatifu anaweza kuachilia madaraka. Sheria ya Kanisa No. 332#2 inaeleza kuwa masharti mawili ya Baba Mtakatifu kuachilia madaraka ya kuliongoza Kanisa, kwanza, ni kufikia uamuzi huo yeye mwenyewe kwa uhuru na kwa hiari yake. 


Pili, ataamke waziwazi juu ya uamuzi wake wa kuachilia madaraka. Baba Mtakatifu anaweza kuachilia madaraka pale anapopoteza uwezo wa kuongoza au inapotokea afya yake ikatetereka na hivi kushindwa kutimiza majukumu yake kikamilifu. Sababu iliyopelekea Baba Mtakatifu Benedikto XVI, ambaye tarehe 16 Aprili atatimiza miaka 85, kuachilia madaraka, kama alivyoeleza mwenyewe ni kutokana na kutetereka kwa afya yake. Akitangaza hatua yake ya kuachilia madaraka aliyoisoma kwa lugha ya kilatini, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alisema:


“Ndugu wapendwa,

Nimeweaalika kwa kusanyiko hili la Makardinali (Consistory), siyo tu kwa ajili ya kuwatakatifuza watakatifu watatu, bali pia kuwatangazieni juu ya uamuzi wenye  umuhimu mkubwa kwa maisha ya Kanisa.  Baada ya kutafakari dhamiri yangu mbele ya Mungu tena na tena, nimeona kwa hakika nguvu zangu, kutokana na kuwa na umri  mkubwa, hazitoshi kuweza kutimiza utume wa Upapa kikamilifu. Najua wazi kwamba utume huu, kutokana na umuhimu wa hulka yake ya Kiroho, unapaswa kutekelezwa si tu kwa maneno na matendo, bali pia kwa sala na mateso. Hata hivyo, katika ulimwengu wa leo, unaokumbwa na  mabadilikko makubwa na kutikiswa na  maswali yenye umuhimu wakina mintarafu maisha ya imani, ili kuongoza mashua ya Petro na kutangaza Injili, nguvu ya akili na mwili ni vya lazima, nguvu ambazo  katika kipindi cha miezi michache iliyopita zimenipungua kiasi cha kugundua kutokuwa na uwezo wa kutekeleza kikamilifu utume niliokabidhiwa. Kwa sababu hiyo, nikijua wazi uzito wa tendo hili, kwa uhuru kamili, natamka kuachia utume wa Askofu wa Roma, Halifa wa Mtume Petro, ambao nilikabidhiwa na Makardinali tarehe 19 April 2005, hivi kwamba kuanzia tarehe 28 Februari 2013, saa 2.00 usiku Kiti cha Roma, Kiti cha Mtume Petro kitakuwa wazi na mkutano wa kumchagua Baba Mtakatifu mpya (conclave) unapaswa kuitishwa na wale walio na mamlaka hayo.

Ndugu wapendwa, ninawashukuru sana kwa upendo wa kazi ambazo mlinisaidia katika utume  wangu na ninaomba radhi kwa mapungufu yangu yote. Na  sasa, tulikabidhiwa Kanisa Takatifu chini ya ulinzi wa Mchungaji Mkuu, Bwana Wetu Yesu Kristo, na tumwombe Mama yake Mtakatifu Maria, ili awasaidie Mababa Kardinali kwa maongezi yake ya kimama katika kumchagua Baba Mtakatifu mpya. Kwa upande wangu, ningependa katika siku zijazo kulihudumia Kanisa Takatifu la Mungu kwa njia ya maisha ya sala.”

Kutoka VATIKANO,  10 FEBRUARI 2013

BENEDICTUS PP XVI

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu kuachilia madaraka.  Historia inaonesha kuwa Baba Watakatifu kati ya  sita (6) na kumi (10) wamekwishaachia nafasi hiyo. Hawa ni pamoja na  Klementi I (92-201), Pontiano (230-235), Siriakusi, Marsellino (296-304), Martin I (649-655), Benedikto V (964), Benedikto IX (1032-1045) Gregori VI (1045-1046) Celestino V (1294) na Gregori XII (1106-1415).

Friday, January 25, 2013

Siku kuu ya Uongofu wa Mtume Paulo

Sikukuu ya Wongofu wa Mtume Paulo ni sikukuu inayoadhimishwa katika mwaka wa kiliturujia Januari 25, ikinukuu uongofu wake. Mbali na kanisa Katoliki, sikukuu hia pia inaadhimishwa na makanisa mbalimbali ya Mashariki Orthodox, Oriental Orthodox, Anglikana na makanisa ya Kilutheri. Kutokana na kuadhimishwa na makanisa haya mbalimbali, sikukuu hii inakua ni hitimisho la wiki ya maombi ya kuombea Umoja wa Wakristu duniani. Wiki hii ya maombi hufanyika kila mwaka kuanzia Januari 18 mpaka Januari 25


Mtakatifu Paulo alizaliwa kati ya miaka 7-10 BK katika familia ya Kiyahudi ya kabila la Benyamini (Israeli) na madhehebu ya Mafarisayo iliyoishi katika mji wa Tarsus (kwa sasa mji huo uko sehemu ya kusini mashariki ya nchi ya Uturuki).
Jina lake la kwanza (la Kiebrania) lilikuwa Sauli, lakini kadiri ya desturi ya wakati ule alikuwa pia na jina la Kigiriki: Paulos kutoka Kilatini Paulus. Mwenyewe alikuwa na uraia wa Roma kama wananchi wote wa Tarsus. Angali kijana alisomea ualimu wa Sheria (yaani wa Torati) huko Yerusalemu chini ya mwalimu maarufu Gamalieli wa madhehebu ya MafarisayoAkishika dini yake kwa msimamo mkali akawa anapinga Ukristo kwa kuwakamata, kuwatesa na hata kuwaua Wakristo, kama vile Stefano Mfiadini mpaka alipotokewa na Yesu Kristo mfufuka akiwa njiani kwenda Damaski (kwa umuhimu wake katika historia ya wokovu habari hii inasimuliwa mara tatu katika kitabu cha Matendo ya Mitume: 9:1-19; 21:12-18 na 22:5-16). Jibu lake kwa Yesu lilikuwa (Mdo 22:10): "Nifanye nini, Bwana?"

Baada ya Wongofu na baada ya kufanya utume katika mazingira ya Kiarabu, Tarsus na Antiokia alianza kufanya safari za kitume, akienda mbali zaidi na zaidi, akilenga kumhubiri Yesu mahali ambapo bado hajafahamika, hata Hispania.
Ilikuwa kawaida yake kuanzisha Kanisa katika miji mikubwa ili toka huko ujumbe ufike hadi vijijini.
Muda wote wa utume wake Paulo alipambana na dhuluma kutoka kwa Wayahudi wenzake na matatizo mengine kutoka Wakristo wenye msimamo tofauti na wa kwake hasa kuhusu haja ya kufuata masharti ya Agano la Kale ili kupata wokovu.
Hatimaye alikamatwa na wapinzani wake Wayahudi mjini Yerusalemu, lakini askari wakoloni walizuia asiuawe. Baada ya hapo alilazimika kukaa gerezani akisubiri hukumu ya Dola la Roma, kwanza Kaisaria Baharini miaka miwili, halafu akakata rufaa kwa Kaisari akapelekwa Roma, alipofika mwaka 61 akakaa miaka miwili tena kifungo cha nje katika nyumba ya kupanga.

Aliuawa nje ya kuta za Roma kwa kukatwa kichwa wakati wa dhuluma za Nero kati ya mwaka 64 na 67 B.K. Kati ya barua nyingi alizoandikwa kwa makanisa ya Thesalonike, Korintho, Galatia, Roma, Filipi, Kolosai,Efeso, kwa viongozi Wakristo kama Timotheo na Tito, tena kwa Filemoni, katika Agano Jipya zinatunzwa 13. Ukubwa na ubora wa mchango wa Paulo unaeleweka tukizingatia kwamba alifanya kazi na kuandika kabla ya vitabu vya Agano Jipya kupatikana. Ndiye aliyeanza kuliandika akipanua mawazo aliyoyapokea katika Kanisa kwa kuzingatia Agano la Kale na mang’amuzi yake mwenyewe.










Saturday, January 12, 2013

Tafakari ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana ni sikukuu yetu. Ni sikukuu inayotukumbusha ubatizo wetu. Tunapofanya sherehe hii, swali linalokuja kichwani mara moja ni hili: ubatizo wa Yohane ni ubatizo wa toba, iweje Yesu asiye na dhambi abatizwe? Yesu mwenyewe anajibu swali hili katika Injili ya Matayo. Wakati Yohane anasitasita kumbatiza, Yesu anamwambia:“Kubali sasa hivi; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote“ (Mt 3: 15).

Yesu anataka “kutimiza haki yote“. Katika kutwaa mwili anatwaa ubinadamu dhaifu, na katika ubatizo wake anatwaa dhambi ya ulimwengu. Anataka “kutimiza haki yote“, ile haki ambayo wazazi wetu wa kwanza wangepaswa kuitimiza; yaani, kuisikiliza sauti ya Mungu na kutimiza mapenzi ya yule aliyewaumba. Utii wa Yesu unaifungua mbingu. Mbingu zilizofungwa kwa dhambi, zinafunguliwa kupitia yule aliyekuwa tayari kutimiza haki ya Mungu. Mbingu zinafunguka, ili Mungu apate kumfunua Yesu kama mwana wake mpendwa. Ni mwana mpendwa kwa sababu yuko tayari kutimiza haki yote ya Mungu. Mbingu zinafunguka ili kwamba sisi kwa kupitia yeye, aliye mlango tufunguliwe mlango wa mbingu kama tutatimiza haki yote. Kuanzia hapo sote tunakuwa wana wa Mungu katika Mwana wa Mungu.



Ubatizo ndiyo mlango wa imani. Imani ndiyo inayotuelekeza kwa Mungu. Wakati wa Kanisa la mwanzo mtu aliulizwa: “Unaomba nini katika Kanisa?“ Naye alipaswa kujibu, “imani“. Imani ndiyo mlango wazi unaotuelekeza kwa Mungu. Imani ndiyo miguu inayotuwezesha kutembea na kuingia kupitia “mbingu zilizofunguka“.

Tuesday, January 8, 2013

Epifania - Siku kuu ya Toleo la Bwana

Kila tarehe 6 Januari,  Kanisa linasheherekea   Siku kuu ya "Toleo la Bwana" inayotambulika kama Epifania. Hii ni Sherehe ambayo Mfalme Masiha anajitambulisha wazi katika Ulimwengu. Injili ya Mathayo 2:1-2 inazungumzia Mamajuzi waliofuata mwongozo wa nyota ili wakamwone Masiha na kumsujudia. Ni kwa njia ya nyota, Mamajusi wanaweza kufika mahali alipokuwa na wakaweza kumsujudia na kumpatia zawadi zao. Kumbe Yesu Kristo Masiha ni nyota inayaangaza na kuongoza maisha yetu mpaka mwisho wa nyakati hadi kufika mbinguni. Katika Siku kuu ya Krismasi tarehe 25 Disemba, Kristo anajitoa katika watu ulimwenguni. Siku kuu ya Toleo la Bwana yaani "Epifania" Mamajusi wanawakilisha watu wote ulimwenguni wanaojitolea kwa Bwana kwa kumwabudu, kumwamini na kumsujudia

Wednesday, January 2, 2013

MIMBARI ZILIZOSIMAMISHWA NA MAENDELEO YA KISASA


“Kama Mt. Paulo angeishi leo”, anasema Mwenyeheri Giacomo Alberione, mwanzilishi wa watawa wa Mtakatifu Paulo, “angefanya bidii ya kutumia mimbari za juu zaidi zilizosimamishwa na maendeleo ya kisasa: uchapishaji, sinema, redio, televisheni”. Wakati Mwenyeheri Giacomo akisema hayo, na mpaka mauti ilipomfika, ulimwengu ulikuwa bado haujajizamisha katika matumizi ya mawasiliano ya kisasa zaidi kama intaneti. Mwenyeheri Alberione amefariki mwaka 1971 wakati mapinduzi ya mtandao yameshika kasi miaka ya 90 baada ya mwanasayansi Tim Berners-Lee wa Uingereza kugundua matumizi ya mtandao mnamo mwaka 1989 kwa namna tunayokuwa nayo leo.

Katika ulimwengu wa kisasa, njia za mawasiliano ya jamii: magazeti, televisheni, radio, intaneti n.k, zinabaki kuwa “mfereji” mpana, wenye nguvu na wenye uwezo wa ajabu katika kufikisha ujumbe na kushawishi mwelekeo wa jamii karibu juu ya kila jambo. Mfereji huu pia umethibitisha kuwa na uwezo wa kupitisha “maji masafi” na hata “maji machafu” pia.

Intaneti, kama ilivyo kwa kila jambo na kila kitu, katika yenyewe haina tatizo. “ Hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake” (Rum. 14:14). Uzuri au ubaya wa kila jambo unajidhihirisha katika matumizi. Mwanadamu kupitia paji la akili, mang’amuzi na ubunifu anaweza kuendeleza kazi ya uumbaji au kuiharibu. Njia za mawasiliano ya kijamii zinapewa sura na mwanadamu pale anapozitumia katika kufikisha ujumbe kwa jamii

Mwanadamu anaweza, katika kuzitumia njia hizi, akaifikishia jamii sura ya kutisha na kukatisha tamaa au sura ya matumaini na yenye kuweza kurahisisha ujenzi wa dhamiri ya jamii. Lakini hata pale inapotokea kuwa njia na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinawasilisha sura isiyopendeza kwa kufikisha ujumbe usio sahihi na wa kubomoa badala ya kujenga, hatupaswi kuvikimbia. Kwa sababu hii ni njia, na hivi ni vyombo visivyoepukika vya mawasiliano ya haraka. Ni umuhimu huu ndiyo unaotufanya kuvitumia ili kuonesha upande mwingine, yaani jinsi vyombo hivi vinavyoweza kutumika kujenga na kuielimisha jamii.

Tusipovitumia vyombo vya mawasiliano ya kijamii kupitishia “maji safi”, wale wanaoutumia kupitishia “maji machafu” wanazidi kudhihirishia kuwa hawana muda wa kupoteza na kubweteka. Wako kazini! Na hiyo ndio kazi yao na lengo lao!

Tusipoutumia mfereji huu kupitishia “maji safi” tutakuwa pia tunawanyima fursa wale wote ambao wangependa kuangalia kwa makini pande mbili za sarafu, tena kwa haraka kupitia njia hii ya mawasiliano. Zaidi sana tutakuwa tunawanyima wale wote ambao wanatumia vyombo vya njia za mawasiliano kupata fursa mbadala inayoweza kuwasaidia kujua, kupima, kulinganisha lipi ni sahihi na lipi si sahihi na kisha kuchagua ni njia ipi wafuate wakiongozwa na uhuru wa utashi na dhamiri zao

Kanisa linavipa vyombo vya mawasiliano ya jamii umuhimu mkubwa. Hii ni kwa sababu vina nafasi muhimu katika uinjilishaji. Zaidi ya hayo, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinawasaidia waamini kupata habari mbalimbali juu na hata dhidi ya imani  yao jambo linalowasaidia kukomaa katika safari yao ya imani.

Kanisa la karne za mwanzo lilijikuta pia likikabiliwa na changamoto za wakati wake, nyingi zikifanana karibu na hizi za nyakati zetu, hususani katika hitaji la kukuza uwezo wa kupambanua na kuchagua jambo lipi ni la kweli na sahihi katika elimu na mtaala wa ulimwengu wa “kipagani”. Ikumbukwe kuwa wakati wa kipindi cha Kanisa la mwanzo na hasa wakati wa kipindi cha Mababa wa Kanisa wa karne ya nne na ya tano, mtaala wa elimu ya wakati huo ulikuwa ule wa shule za “kipagani”. Katika shule hizi walisoma wapagani na wakristo pia. Kazi za fasihi ziliyosomwa mashuleni zilikuwa ni za “kipagani”. Kazi za fasihi, historia na falsafa zilizotumika wakati huo zilikuwa zile za elimu ya kilatini na kiyunani (classical), za akina Homer, Tucidide, Cicero, Virgil, Plato, Aristotle n.k.  Waalimu maarufu wa kipagani kama Libanio ndio waliowafundisha Mababa wa Kanisa maarufu kama Yohane Krisostom.  

Msisitizo wa Kanisa la wakati huo ulikuwa ni juu ya katekesi ya imani na umakini wa wanafunzi wakristo katika kuweza kupambanua yale wanayojifunza shuleni. Mababa wa Kanisa ambao walikuwa ni “makatekista” mashuhuri waliwasisitizia wanafunzi wakristo kujifunza kuchuja yale waliyojifunza shule kwa mwanga wa imani yao

Mt. Basili Mkuu, kwa mfano, katika hotuba yake  kwa vijana anasema: Kwa upande wetu, ni lazima tuhudhurie mihadhara hii tukiiga mfano wa nyuki. Nyuki hawatui juu ya kila ua pasipo kuchagua, na hata juu ya maua yale ambayo juu yake wanatua hawachukui kila kitu, wanapokuwa tayari wamechukua kile kinachofaa, wanaacha kile kisichofaa: hata sisi, kama tuna hekima, tukishachukua kutoka kwao (waandishi wapagani) kile kinachotufaa, na kinachopatana na ukweli, tunaacha makombo ( Hotuba kwa vijana, 4).

Kimsingi, Mababa wa Kanisa waling’amua kuwa si kila kilichomo katika mafundisho ya kipagani ni ubatili. Waling’amua kuwa ilikuwamo hekima pia katika mafundisho hayo. Ndiyo maana, Kanisa halikuacha kutoa elimu ya falsafa ya Wayunani kwa sababu liliamini kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kuweza kufikisha ujumbe wake kwa jamii ya wasomi wa wakati huo. Mt. Justino (c. 100-165) anasema, kama Agano la Kale linatuelekeza kwa Kristo kama jinsi taswira inavyotuelekeza kwenye uhalisia inaouwakilisha, basi falsafa ya kiyunani nayo inatuelekeza  kwa Kristo na Injili, kama jinsi sehemu ya kitu isivyokamilika bila kuungana na kitu kizima. Kadiri ya Mt Justino , Agano la Kale na falsafa ya kiyunani ni njia mbili zinazotuelekeza kwa Kristo.

Umuhimu wa kuwasilisha na kufafanua imani yetu na mafundisho ya Kanisa ndio inayotuvuta kuingia ulingoni ili nasi tuweze kutoa mchango watu, hata kama ni mdogo, kupitia “mimbari” hii ya kisasa.

Amepata kuandika Svetonio, mwanahistoria wa kirumi (c. 69-122) juu ya Kaisari Tito Flavio aliyetawala kati ya mwaka 79-81 BK (Tito alikuwa  moja ya makaisari wa Kirumi walioheshimiwa na kupendwa sana)   akisema kuwa Tito alijiwekwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa siku haipiti bila kutenda tendo jema lenye kuleta faraja na matumaini kwa yeyote anayemwendea.  Siku moja akiwa mezani wakati wa chakula cha jioni, Tito aligundua kuwa siku hiyo ilipita na hakuwa amefanya tendo lolote jema. Ghafla alipaaza sauti akasema: “Amici, diem perdidi!” Rafiki zangu, nimepoteza siku! Tusingependa nasi kupoteza fursa ya kutumia mimbari hii ya teknolojia ya kisasa.

Na Fr. Ray Saba