Sikukuu ya Ubatizo wa
Bwana ni sikukuu yetu. Ni sikukuu inayotukumbusha ubatizo wetu. Tunapofanya
sherehe hii, swali linalokuja kichwani mara moja ni hili: ubatizo wa Yohane ni
ubatizo wa toba, iweje Yesu asiye na dhambi abatizwe? Yesu mwenyewe anajibu
swali hili katika Injili ya Matayo. Wakati Yohane anasitasita kumbatiza, Yesu
anamwambia:“Kubali sasa hivi; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote“
(Mt 3: 15).
Yesu anataka “kutimiza haki yote“. Katika kutwaa mwili
anatwaa ubinadamu dhaifu, na katika ubatizo wake anatwaa dhambi ya ulimwengu.
Anataka “kutimiza haki yote“, ile haki ambayo wazazi wetu wa kwanza wangepaswa
kuitimiza; yaani, kuisikiliza sauti ya Mungu na kutimiza mapenzi ya yule
aliyewaumba. Utii wa Yesu unaifungua mbingu. Mbingu zilizofungwa kwa dhambi,
zinafunguliwa kupitia yule aliyekuwa tayari kutimiza haki ya Mungu. Mbingu
zinafunguka, ili Mungu apate kumfunua Yesu kama mwana wake mpendwa. Ni mwana
mpendwa kwa sababu yuko tayari kutimiza haki yote ya Mungu. Mbingu zinafunguka
ili kwamba sisi kwa kupitia yeye, aliye mlango
tufunguliwe mlango wa mbingu kama tutatimiza haki yote. Kuanzia hapo sote
tunakuwa wana wa Mungu katika Mwana wa Mungu.
Ubatizo ndiyo mlango wa
imani. Imani ndiyo inayotuelekeza kwa Mungu. Wakati wa Kanisa la mwanzo mtu
aliulizwa: “Unaomba nini katika Kanisa?“ Naye alipaswa kujibu, “imani“. Imani
ndiyo mlango wazi unaotuelekeza kwa Mungu. Imani ndiyo miguu inayotuwezesha
kutembea na kuingia kupitia “mbingu zilizofunguka“.
No comments:
Post a Comment