Mtakatifu wa siku ya leo

Februari 8, Kanisa huadhimisha maisha ya Mtakatifu  Josephine Bakhita, Dada Canossian ambaye alitekwa nyara na kuuzwa utumwani akiwa nchini Sudan.                                                                          
Mt. Bakhita Josephine alizaliwa mwaka 1869, katika kijiji kidogo katika eneo la Darfur nchini Sudan. Yeye alitekwa nyara wakati akifanya kazi katika mashamba na familia yake na hatimaye kuuzwa utumwani. Watekaji wake walimuuliza jina lake lakini kwa kuwa alijawa na hofu kubwa alishindwa kukumbuka. Hivyo watekaji wakamuita "Bakhita," ambayo ina maana ya "bahati" kwa Kiarabu.
Mt. Bakhita alikuja jaliwa bahati sana, lakini miaka ya kwanza ya maisha yake haikushuhudia hilo. Kama mtumwa alipata mateso makali sana na wamiliki wake mbali mbali ambao walimtupia majina, wakampiga na kumkata. Katika wasifu wake anabainisha teso moja la kutisha wakati ambapo mmoja wa wamiliki wake alimkata mara 114 na akamwaga chumvi katika majeraha yake ili kuhakikisha kwamba makovu yanabaki. "Nilihisi Mimi ningelienda kufa wakati wowote, hasa wakati wakisugua majeraha yangu na chumvi," Bakhita aliandika.

Alivumilia mateso yake kwa ushujaa ingawa hakumjua Kristo au asili ya ukombozi na neema katika mateso. Mt. Bakhita pia na mshangao fulani kwa maumbile ya dunia na muumba wake. "Ukiangalia jua, mwezi na nyota, nikajisemea: 'Nani anaweza kuwa Bwana wa mambo haya mazuri?' Na nilihisi hamu kubwa ya kumwona,kumjua yeye na kumtolea heshima. "

Baada ya kuwa ameuzwa jumla ya mara tano, Bakhita alinunuliwa na Callisto Legnani, Balozi Italia huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Miaka miwili baadaye, mmiliki huyo alimchukua Bakhita huko Italia ili afanye kazi ya kulea watoto kwa rafiki yake Augusto Michieli.  Yeye Augusto, kwa upande wake, alimtuma Bakhita kuongozana na binti yake shule huko Venice.  Shule hiyo ilimilikiwa na Masista watawa wa Canossian.

Mt. Bakhita alijihisi amepewa wito wa kujifunza zaidi kuhusu Kanisa, akabatizwa na jina la "Josephine Margaret." Wakati huo huo, Augusto Michieli alitaka kumchukua Mt. Josephine (Bakhita) na binti yake ili awarudishe Sudan, lakini Mt. Josephine alikataa kurejea.

Kutokana na hali hiyo ya kupingana na kutokubaliana Mt. Bakhita  alipelekwa mahakamani Italia ambapo Mahakama iliamuru kwamba Mt. Josephine Bakhita anaweza kubaki nchini Italia kwa sababu yeye alikuwa mwanamke huru. Hali ya Utumwa haikutambuliwa nchini Italia na alikuwa pia ni kinyume cha sheria nchini Sudan tangu kabla Mt. Josephine hajazaliwa.

Mt. Josephine alibakia nchini Italia na aliamua kujiunga na Masista watawa wa Canossians mwaka 1893. Alipata taaluma yake mwaka 1896 na alitumwa huko Italia ya Kaskazini, ambapo alijitolea maisha yake kusaidia jamii yake na kuwafundisha wengine kumpenda Mungu.

Alijulikana kwa tabasamu, upole wake, na utakatifu wake. Aliwahi kunukuliwa akisema, "Kama ningebahatika kukutana na wafanyabiashara wa utumwa walioniteka nyara na kunipa mateso makali, ningewapigia magoti na kubusu mikono yao, kwa maana kama kwamba isingalitokea hivyo, nisingalikuwa Mkristo na mwenye dini leo. "

Mt. Josephine alifanywa mwenye heri mwaka 1992 na utakatifu ukafuata muda mfupi baada ya Oktoba 2000 baada ya kutambuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II. Yeye ni mtu wa kwanza kutambulika kama Mtakatifu na anafahamika kama Mtakatifu mlinzi wa nchi ya Sudan.


========================================================================
Tarehe 6 Februari, Kumbukumbu y Mtakatifu Paulo Miki na Watakatifu wenzake 26 wafia dini. Mtakatifu Paulo Miki mwenye asili ya Japan alikua Mkatoliki wa Shirika la Jesuit. Alifariki kama mfia dini (Februri 5, 1597) akiwa kati ya wale wafia dini 26 wa nchi ya Japan ambao Kanisa pia limewatambua kama Watakatifu. Hii ilitokea katika mji uliofahamika haswa kwa kuwa na idadi kubwa sana ya ukatoliki kutokana na jitihada za M-Jesuit Mtakatifu Francis Xavier.

Mt. Paul Miki alizaliwa kwenye familia yenye utajiri mkubwa. Alipata elimu yake kupitia shirika la Jesuit huko Azuchi na Takatsuki nchini Japan. Rasmi alijiunga na shirika hilo la Jesuit na kufahamika na wengi kama mhubiri mashuhuri aliyefanikiwa kuwaleta wengi katika imani ya Kristo ya Kanisa Katoliki.  kutokana na hofu ya kuenea kwa kasi imani ya katoliki nchini Japan, Watawala wa Japan walifanikiwa kuwafunga Mt. Miki pamoja na wenzake. Yeye pamoja na wenzake wakatoliki waliamuriwa kutembea maili 600 sawa na kilomita 966 kutoka Kyoto mpaka Nagasaki. Kutokana na Imani yao kubwa waliimba mwimbo wa kumtukuza Mungu njia nzima. Walipofika Nagasaki (Mji wenye Idadi kubwa ya Wakatoliki nchini Japan), Mtakatifu Miki alisulubiwa msalabani kama Kristu mwaka 1597 February.  Akiwa msalabani akatoa mahubiri yake ya mwisho akisisitiza kuwa amewasamehe waliomsulubu na kusisitiza kuwa yeye ni MJapan. Yeye alisulibiwa pamoja na wenzake 26 na mnamo mwaka 1862, Baba Mtakatifu Papa Pius IX aliwatambua kama Watakatifu




Akihubiri wakati yuko msalabani alisema:
 “Hukumu kwangu na wenzangu inasema sisi tumekuja Japan kutoka nchini Filipino, lakini sikutokea nchi nyingine bali mimi ni mjapani kamili. Sababu moja tu ya mimi kusulubiwa ni kwamba nimefundisha Injili ya Kristo. Ni kweli nimefundisha Injili hiyo.  Ninamshukuru Mungu ninakufa kwa jambo hilo. Naamini kwamba nimefundisha ukweli kabla ya mauti yangu. Ninafahamu mnaniamini lakini pia nataka niwaambie mara nyingine, ninamuomba Kristu awasaidie muwe na furaha. Nina mtii Kristu na kwa mfano wake ninawasamehe walioniua. Siwachukii bali namuomba Mungu awasamehe na ninatumai damu yangu itawaangukia wakristu wenzangu kama mvua yenye faida”





=======================================================================


Februari 3, Kumbukumbu ya Mtakatifu Blaise. Wakatoliki wengi waweza kukumbuka siku kuu ya Mt. blaise kutokana na upokeaji wa baraka za uponyaji wa magonjwa mbalimbali lakini haswa magonjwa ya Koo katika Misa inayoadhimisha ukumbusho huo. Mishumaa miwili inayoshikiliwa pamoja inawekwa kwenye koo ya mgonjwa huku Baraka za uponyaji zikitolewa. Tukio hili la ulinzi wa magonjwa ya koo kupitia maombi ya Mt. Blaise yanatokana na matendo ya miujiza ya uponyaji aliyofanya Mtakatifu huyu haswa lile la kumponya mtoto aliyekaribia kupoteza maisha yake kwa kukabwa koo na mfupa wa samaki.


Mt. Blaise alikua ni Askofu wa Sebastia huko Armenia ambaye alifariki kama mfia Dini katika utawala wa Licinius mnamo karne ya nne (4). Mt. Blaise alizaliwa katika familia tajiri lakini yenye maadili iliyomlea kama mkristu toka utotoni. Baada ya kufanywa Askofu, yakaanza mateso makali kwa Wakristu yakifanywa na wapagani. Alipata ujumbe kwa Mungu akaambiwa akimbilie milimani ili kuyakwepa mateso hayo waliyoyapata wakristu. Siku moja wanaume waliokuwa wakiwinda walikuja ligundua pango huko mlimani lililozungukwa na wanyama pori walioshambuliwa na magonjwa mbali mbali. Katikati yao alitembea Mt. Blaise asiyeonekana kujawa na woga akiwazungukia na kuwatibu wanyama hao. Walipogundua kuwa ni Askofu walimkamata ili wakamfungulie mashtaka. Wakiwa njiani, kupitia maajabu yake alifanikiwa kumshawishi Mbwa Mwitu kumwachia nguruwe ambaye alimilikiwa na mwanamke maskini asiye na mali. Mt. Blaise alihukumiwa kifo cha kushindishwa njaa. Wakati yu kifungoni, mwanamke maskini aliyesaidiwa aliweza kupenyeza gerezani na kufanikiwa kumletea mshumaa na chakula. Hatimaye Mt. Blaise alikuja kuuawa na mtawala wa pale kwa kukatwa kichwa. 

“Matendo ya Mt. Blaise”
Mt. Blaise ambaye alisoma filosofi katika ujana wake alikua ni Daktari katika mji wa kuzaiwa Sebaste huko Armenia. Alifanya kazi yake ya tiba kwa uwezo wa ajabu wa miujiza, upendo na ucha Mungu. Baada ya Askofu wa mji wake kufariki aliteuliwa kumrithi na hivyo kutambuliwa na watu wote. Ucha Mungu wake ulithibitishwa na miujiza mingi. Kutoka kila kona watu wengi walimfuata kupata tiba za kiroho na kimwili. Hata wanyama walimwijia kupata tiba. Mnamo mwaka 316, Agricola, Gavana Cappadocia na Armenia, baaya ya kufika Sebastia akibeba amri kutoka kwa Mfalme ya kuwakatama na kuwaua wakristu alifanikiwa pia kumkamata Askofu Blaise. Akiwa anapelekwa gerezani, Mama mmoja alimpeleka mwanaye wa pekee miguuni mwa Mt. Blaise. Mwanaye huyu aliyekaribia kufa kwa kukabwa na mfupa wa samaki kwenye koo aliweza kuponywa mara moja. Gavana Agricola baada ya kushindwa kumfanya Mt. Blaise amkane Kristu na Imani yake akaamua kumpiga fimbo na kutoa amri ya kukatwa kichwa. Mt Blaise alikufa kama mfia dini akimshuhudia Kristu


Tarehe 3 Februari, kumbukumbu ya Mtakatifu Ansgar. Mt. Ansgar, “Mtume wa Kaskazini” alizaliwa karibu na Corbie, Ufaransa mnamo mwaka 801 KB. Aliingia katika utawa wa Benedikto na kuwa mwalimu na mhubiri wa nguvu. Alitumwa kama mshionari kule Denmark. Kwa kipindi cha miaka mitatu alifanya kazi ya kimishionari akiwahubiria watu lakini kwa shida sana. 
Wakati nchi ya Sweden ilipohotaji wamishionari zaidi, Ansgar alifunga safari lakini akisindikizwa na mtawa mwingine. Njiani alikamatwa na majangiri na kupata mateso makali lakini hatimaye alifanikiwa kufika Sweden. Kabla hajamaliz tu miaka miwili, Ansgar aliitwa na kufanywa Askofu Mkuu wa Hamburg mwaka 831. Ni katika nafasi hii muafaka Ansgar alifanikiwa kutuma wamisionari wa kwanza huko Hanover nchini Ujerumani. 

Katika kipindi cha miaka 13, Mt. Ansgar alifanya kazi na kusali mjini Hamburg. Alipata umaarufu mkubwa kwa uwezo wake wa kuhubiri, kwa upendo wake kwa maskini na wagonjwa na haswa kwa upole na maisha yake ya kiroho na kusali. Bahati mbaya janga jingine kubwa likatokea, mwaka 1845 Hamburg ilivamiwa na watu wa Kaskazini na kuteketea  kabisa kwa moto.Kutokana na hilo Ansgar alishuhudia waumini wakirudi katika dini ya kipagani na kuukacha Ukristo. Lakini hakukata tama akaendelea kuhubiri.

Mnamo mwaka 854, Mt. Ansgar aliteuliwa kuwa skofu Mkuu wa Bremen na kuanza kazi mpya ya kimisionari nchini Sweden na Denmark. Akamuomba Mungu muujiza mmoja tu, kwamba Mungu amfanye awe mtu mwema. Ndani ya moyo wake alitamani sana kutoa maisha yake kwa ajili ya Imani na kuonyesha upendo wake kwa njia ya Mfia Dini. Tofauti na mapenzi yake, Ansgar alifariki kwa amani huko Bremen Februari 3, 865 na kuzikwa Parokiani. Baada ya kifo chake, Sweden ikarudia imani yake ya Kipagani.

Mt. Ansgar alikua Padri, Askofu na mhubiri mahiri ambaye wasifu wake uliandikwa na Askofu Rembert aliyemuita Mtakatifu. Heshima hii ilikuja baadae kutambuliwa rasmi na Kanisa baada ya Baba Mtakatifu Papa Nikolas kuthibitisha Utakatifu wake (858).
========================================================================


John Bosco (16 Agosti, 1815  31 Januari, 1888) alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mwanzilishi wa Shirika la Mt. Fransisko wa Sales. Alitumia maisha yake kuwaelimisha watoto na vijana wa mtaani, yatima na vijana wa magereza.  Hakutaka kurekebisha vijana kwa ukali, bali kuwakinga dhidi ya maovu kwa wema. Upendo wake wa ajabu kwa vijana ndio siri ya mafanikio yake ya ajabu katika malezi.
Giovanni Bosco alizaliwa tarehe 16 Agosti 1815 akilelewa na mama yake mjane, baba yake alifariki mwaka 1917 akimuachia mke wake watoto watatu. Ilikuwa ni kipindi cha miaka migumu kutokana na maradhi na njaa, lakini mama yake alijitahidi kuwatunza na kuwalea vizuri.

Alipokuwa na miaka 9 Yohane alipata ndoto ya kinabii iliyomtabiria utume wake kwa vijana. Baadaye Mungu alizidi kumjalia karama nyingi za pekee.
Kufuatana na ndoto hiyo, Yohane aliamua kuwa padri, ingawa hakuweza kusoma hata shule ya msingi kutokana na umaskini wa nyumbani. Ndoto za kuwa Padri alizipata utotoni lakini kaka yake alimpinga vita na kutaka awe mkulima kama yeye. Lakini taratibu mama alimfanyia mpango dhidi ya upinzani wa kaka yake. Wakati huohuo alianza utume wake akitumia vipawa vyake vyaajabu. Alibahatika kukutana na Padri mzee ambaye alimsaidia katika kupata elimu kwenye seminari. Kwa shauri la Padri Yosefu Cafasso tarehe 30 Oktoba 1835 aliingia seminari ya Chieri. Tarehe 3 Novemba 1837 alianza masomo ya teolojia, na tarehe 29 Machi 1841 akapewa daraja takatifu ya ushemasi, na tarehe 5 Juni 1841 upadri huko Torino.

Katika kazi yake ya Upadre, pia alifundisha Katekisi kwa vijana, alitembelea wafungwa na kusaidia katika parokia mbali mbali nchini. Huko Torino kulikuwa na watoto 7184 chini ya umri wa miaka 10 waliofanya kazi viwandani. Yohane Bosco aliwatafuta ili kuwasaidia kijamii na kidini. Pamoja na Padri Cafasso alitembelea magereza akashtuka kuona hali ya wafungwa vijana. Kwa wema wake aliwavuta kumuahidia wamuendee mara baada ya kutoka. Muda mfupi baadaye vijana walikuwa wengi hivi hata akahitaji msaada wa mapadri watatu na vijana wakubwa kadhaa.

Hatimaye tarehe 12 Aprili 1846 alipata nafasi kwa vijana wake na kununua kibanda na kiwanja huko Valdocco. Mama yake pia aliamia katika kibanda hicho na wakasaidiana kutafuta na kuelea watoto yatima
Mwaka 1854 alianzisha shirika la mapadri kwa utume wa vijana (kifupisho chake ni SDB). Miaka 10 baadaye alianza ujenzi wa mahali patakatifu pa Bikira Maria - Msaada wa Wakristo (ndivyo alivyopendelea kumuita mama wa Yesu). Mwaka 1872, pamoja na Maria Domenica Mazzarello, alianzisha shirika la Mabinti wa Bikira Maria Msaidizi, ili walee wasichana kwa roho ileile.
Akiwa kama mwanzilishi wa Shirika la Mt. Fransisko wa Sales, mwaka 1875 alianza kutuma Wasalesiani wa kwanza huko Argentina, na wakati huohuo alianzisha kundi la watawa wasaidizi aliowaona kama Wasalesiani wa nje.
Yohane Bosco alifariki tarehe 31 Januari1888. Msiba wake ulihudhuria na maelfu ya watu. Mara baada ya kifo, jamii kubwa ilitamani zianze taratibu ya kumfanya Yohane Bosco kutambuliwa kama Mtakatifu
Papa Pius XI alimtangaza mwenye heri tarehe 2 Juni 1929 na mtakatifu tarehe 1 Aprili 1934 akipewa jina kama “Baba na Mwalimu wa Vijana. Sikukuu yake ni tarehe 31 Januari.
========================================================================

Tarehe 28 January ni kumbukumbu ya Mtakatifu, Mwalimu wa Kanisa Thomas Aquinas.
Mtakatifu Thomas Aquinas alikua Padri wa Italia katika shirika la kitawa la Dominika. Mt. Thomas alizaliwa Tarehe 28 Januari akiwa mtoto wa Landolfo, sharifu mwenye asili ya Kilombardi, na mke wake, Teodora. Akiwa mtoto wa miaka 5 tu, alitumwa kuishi na Wabenedikto katika Abasia ya Monte Cassino ili apate malezi ya kitawa.
Alipofikia umri wa miaka 14 alihamia Napoli, aliposoma katika chuo kikuu, karibu na konventi ya Chiesa di San Domenico Maggiore (Napoli). Ingawa alipingwa sana na familia yake, mwaka1244 aliamua kujiunga na shirika la Wadominiko.
Kutokana na ukuu wa akili yake, wakubwa wa shirika hilo walimtuma Paris ili aweze kukamilisha masomo yake, lakini kabla hajafika huko alikamatwa na wanafamilia na kufungwa katika ngome ya baba yake huko Monte San Giovanni Campano alipokaa mwaka mzima, akishinikizwa aoe.
Hatimaye alitoroka au alifunguliwa kutokana na ombi la Papa Inosenti IV. Baada ya kukaa kidogo Napoli na Roma, mwaka 1248 alifika Cologne (Ujerumani) ili kufundishwa na Mtakatifu Alberto Mkuu, mwanasayansi, mwanafalsafa na mwanateolojia wa shirika lake aliyejaribu kulinganisha Ukristo na falsafa ya Aristoteli. Mt. Alberto Mkuu pia anaheshimika na Kanisa kama Mwalimu wa Kanisa
Kuanzia mwaka 1252 alifundisha kwenye Chuo kikuu cha Paris, na baada ya miaka 4 aliweza kufundisha kama Profesa. Mwaka 1259 alirudi Italia na kushirikiana na Papa Urbano IV. Kwa agizo la Papa, Mt. Thomas alitunga na kupanga liturujia yote ya sikukuu mpya ya Corpus Domini (Mwili na Damu ya Kristo) iliyoanzishwa tarehe 8 Septemba 1264).
Halafu alihamia Roma ili kupanga kozi za chuo cha santa Sabina na mwaka 1267, Papa Clemens IV alimuita kwake Viterbo, alipohubiri mara nyingi katika kanisa la Santa Maria Nuova.
Thomas anachukuliwa na Kanisa Katoliki kama mfano bora kwa wale wanaosomea Upadrisho.  Utafiti wa kazi yake, kutokana na maandishi ya Mapapa, unachukuliwa kama ni msingi wa mafundisho kwa wale wanaotafuta kupokea Sakrament za Upadrisho, ushemasi, na vilevile wale walio katika malezi ya kidini na kwa wanafunzi wengine wa taaluma takatifu (Falsafa ya Katoliki, teolojia, historia, liturujia, na kanuni ya sheria ya Kanisa).

Akiwa mmoja kati ya Walimu 35 wa Kanisa, yeye kutokana na upeo wake anachukuliwa na baadhi ya wanateolojia mbali mbali kama Mwalimu wa Kanisa mwenye upeo wa juu zaidi kuliko wote. Mchango wake mkubwa zaidi katika Kanisa Katoliki ni Maandishi yake haswa yale yanayofahamika kama “Summa Theology”. 
========================================================================

Tarehe 13 Januari ni Kumbukumbu ya Hiari ya Mtakatifu Hilari wa Poitiers. Hilari wa Poitiers anafahamika kama mwanateolojia, mwanafalsafa na mwandishi. Lakini haswa anaheshimika na Kanisa kama Mtakatifu na Baba wa Kanisa (mafundisho yake yatuwezesha kufahamu mapokeo ya Mitume). Mwaka 1851, Hilari wa Poitiers alipewa na Kanisa heshima kubwa anayoweza kupewa Mtakatifu pale alipofanywa Mwalimu wa Kanisa.

Mtakatifu Hilari alizaliwa katika karne ya 4 (300-368) katika familia ya kipagani. Alipokea elimu nzuri na elimu hiyo aliitumia kujifunza maandiko ya Biblia ya Agano la Kale na Agano Jipya. Matokeo yake aliweza kubatizwa pamoja na familia yake na kupokewa rasmi na Kanisa. Kutokana na elimu yake ya Kanisa na heshima aliyopewa na jamii nzima, alifanywa kuwa Askofu wa Poitiers mnamo mwaka 353.
Alikuja kuifahamu Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli na kuitetea kwa nguvu katika sinodi na mitaguso dhidi ya uzushi wa Waario. Waario walifahamika katika upotoshaji wao wa Utatu Mtakatifu wakipotosha kwamba Kristu yu chini ya Baba, hakuwepo toka mwanzo bali alitengenezwa na Baba hivyo hawezi kuwa sawa na Baba na hawezi kuwa ni Mungu.

Haya ni maandishi ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuhusu Baba wa Kanisa Mt.Hilari

Maelezo ya Mt. Hilari kwa ufupi

========================================================================

Tarehe 2 Januari ni Kumbukumbu ya Watakatifu Basili wa Kaisarea na Gregori wa Nazianzo. Katika Kanisa Katoliki, hawa ni mojawapo ya Mababa wa Kanisa. Mababa wa Kanisa ni jina la heshima ambalo kuanzia karne ya 4, Kanisa Katoliki limewapatia Wakristo wa kale (hadi mwaka 750 hivi), wenye Utakatifu, Elimu na Imani sahihi, ambao mafundisho yao yanawezesha kujua mapokeo ya Mitume

Pia Watakatifu hawa wanajulikana katika orodha finyu wa Watakatifu ambao ni Walimu wa Kanisa. Mwalimu wa Kanisa ni heshima ya juu kuliko zote anazoweza kupewa Mtakatifu anayetambuliwa na Kanisa.  Heshima hii ya nadra sana anapewa Mtakatifu ambaye katika maisha, mafundisho na maandishi yake alionyesha na kueneza mwanga wa pekee katika masuala ya Imani, maadili na maisha ya kiroho

Basili wa Kaisarea (mwaka 329 - 379) alikua Askofu katika mji wa Kaisarea wakati Gregori wa Nazianzo (329 - 390) alikua ni Askofu Mkuu katika mji wa Konstaninopo. Wawili hawa wanajulikana kwa uteolojia wao mkubwa hasa katika utetezi wa teolojia ya Utatu Mtakatifu ambayo ilileta utata mkubwa katika kanisa la mwanzo

=================================================================================

Tarehe 28 Desemba, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Watoto Watakatifu ambao walikufa kama Mashahidi wa Kristu. Hii ilitokana na hofu ya Mfalme Herode aliyehofia kupoteza ufalme wake kutokana na utabiri kwamba atazaliwa Mfalme katika Israel atakayetawala Milele (INJILI YA MATHAYO 2:13-18)


Tarehe 29 Desemba, ni adhimisho la kumbukumbu ya Mtakatifu Thomas Becket Askofu Mkuu wa Canterbury Uingereza kuanzia mwaka 1162 hadi mwaka 1170 alipokufa kama Shahidi wa Kristu baada ya kupingana na Mfalme wa Uingereza kuhusu haki za Kanisa



10 comments:

  1. ASANTE SANA KWA KUTUPATIA HISTORIA ZA WATAKATIFU. HUU UKURASA UTAKUWA UNAANDIKA WATAKATIFU WOTE WA SIKU HIYO AU UTAKUWA UNAKUWA 'UPDATED' BAADA YA SIKU NGAPI? MAANA LEO NI SIKUKUU YA MT. THOMAS WA AQUINO LAKINI BADO NAONA KUNA HABARI ZA MTAKATIFU WA TAREHE A13 JANUARY 2013

    ReplyDelete
  2. Tumsifu Yesu Kristu,
    Ukurasa huu unafuata Kalenda ya Roma ambayo imeorodhesha siku ambazo Kanisa linaadhimisha mafumbo ya Kristu, Kumbukumbu na Siku kuu za Watakatifu mbali mbali wanaotambuika na Kanisa. Si Watakatifu wote wanaotambulika na kuheshimika na Kanisa wameorodheshwa katika Kalenda hii.

    ReplyDelete
  3. Ni ukurasa mzuri wenye hekima na busara za kipekee pale tunapoweza kusoma na kuelewa historia za watakatifu wetu.

    Nina shida na Historia ya Mt Yuda Thadei Mtume,Napenda nipate historia yake japo kwa ufupi Nitashukuru kwa ujumla wake.

    ReplyDelete
  4. Kristo!
    Nashukuru sana kwa ukurasa huu. MUNGU awabarikini nyote mnao andaa.

    Naomba kupata historia kamili ya Mtakatifu Thoma wa Aquino, hasa kuhusu yeye kama msimamizi wa vyuo vikuu

    ReplyDelete
  5. Naomba historia ya Mt. Rosalia wa Palermo

    ReplyDelete
  6. TYK Naomba kujua kumbukimbu ya Mt. Yuda Thadei huadhimishwa tarehe ngapi?

    ReplyDelete
  7. shukrani sana kwa historia ya watakatifu. pad. murmi

    ReplyDelete
  8. Naomba mwenye sala ya mt josephine bakhita anitumie

    ReplyDelete
  9. Naomba mwenye sala ya mt josephine bakhita anitumie

    ReplyDelete
  10. Kristu, Asanteni sana kwa kutupatia wasifu wa Watakatifu, Ninaomba sala ya Mt. Thomas wa Acquino nakala ya Kiswahili. Ninawatakia utume mwema, LUBUVA,ELISEI-ILAZO DODOMA

    ReplyDelete