Monday, March 10, 2014

MARIA IMAKULATA

Mafundisho ya Kanisa kuhusu Mama Maria kamwe si mageni bali yalisimamiwa na Kanisa na wakristu wote toka karne ya kwanza baada ya Kristu. Itakua ni vyema kutoa kwa ufupi historia ya fundisho hilo linalomhusu Mama Maria. Kanisa linafundisha kuwa katika kipindi chote cha maisha yake duniani, Mama Maria kwa neema za Mungu hakutenda dhambi wala hakua na doa la dhambi. Kanisa hilo Moja la mitume la Mashariki (Orthodox) na Magharibi (Roma Katoliki) hata baada ya kuvunjika umoja wao mnamo mwaka 1054 karne ya 11, bado linafundisha na kushikilia imani hiyo mpake sasa. Kwa huzuni kubwa Kanisa la magharibi (Roma Katoliki) pia likavunjika karne ya 16 na kutengeneza pande mbili za Waprotestanti na Wakatoliki huku baadhi ya Waprotestanti wakikataa fundisho hilo japo si wote kama ilivyobaki kwa Martin Luther ambaye hakuonyesha kupinga. Heshima aliyokuwa akipewa Mama ikapuuziwa na msaada wake wa kutuombea na kuturudisha kwa mwanaye Kristu ukakataliwa na baadhi ya wakristu. Hivyo basi Kanisa la magharibi likaendelea kugawanyika katika mafundisho yake. Ili wakatoliki wasitetereke katika imani yao juu ya Mama Maria, mnamo mwaka 1854 Baba Mtakatifu Pius IX (Mwenye Heri) kama mrithi wa kiti cha Mtume Petro, kupitia mamlaka aliyopewa ya kufunga na kufungua (Mathayo 16:19) akatangaza kupitia heshima ya kiti hicho yaani ex cathedra fundisho la imani yaani Dogma ambalo humpasa kila mkatoliki kuamini bila kupinga kwa kuwa dogma ni fundisho la Roho Mtakatifu mwenyewe. Hivyo kama Dogma, Mama Maria akatangazwa kuzaliwa bila dhambi ya asili yaani Immaculate Conception. Neno Imakulata (immaculate) maana yake ni usafi usio na doa la uchafu.

Iliwezekana vipi Mama Maria kukingiwa dhambi ya asili na kuishi bila dhambi?

Injili ya Luka inatuambia kuwa malaika Gabrieli anamsalimu Mama Maria kwa salamu ya pekee kabisa akisema "Salamu Maria umejaa Neema, Bwana yu nawe" (luka 1:28). Neema basi ni kitu gani? Neema ni zawadi ya bure itokayo kwa Mungu Baba, zawadi hii kwa mafundisho ya Mtume Paulo ndiyo ituokoayo (Waefeso 2). Hakuna binadamu kwa matendo yake mwenyewe anaweza kuokolewa bila Neema ya Mungu. Tukiendelea kutafakari salamu ya malaika Gabriel, tunakutana na neno "umejaa neema". Neno kujaa linaashiria kipimo kamili kabisa kisichokua na upungufu hata kidogo. Hivyo Mama Maria alijazwa Neema ya pekee kuliko ya mtu yeyote yule. Neema hiyo ndiyo iliyomfanya aweze kushinda majaribu yake yote. Lakini Je, jambo hili ameweza kulifanya kwa nguvu zake mwenyewe. HAPANA, Mama Maria alifahamu kwamba naye aliokolewa kwa kukingiwa dhambi hivyo anasema katika mwimbo wake "Magnificat " akisema “Na roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu” (Luka 1:47). Neema itokayo kwa Bwana ndio iokoayo. Mama Maria ni binadamu na ni kiumbe cha Mungu kama sisi wote tulivyo. Lakini kwa ule utayari wake katika kushiriki ule mpango wa Mungu wa kuikomboa Dunia kwa kukubali kwa hiari na kusema NDIYO (..Na iwe kwangu kama ulivyosema (Luka 1:38) na kwa neema tele za Kristu mwanaye, basi Mungu toka milele alimpatia Maria neema hiyo kabla hata hajamuumba. Ndipo wanakoliki tunapokiri kwamba Mama alikingiwa dhambi ya asili kabla hata ya kuumbwa yaani Immaculate Conception. Japo Maria ni binadamu kamili kama sisi, tofauti ni kuwa sisi tunazaliwa na dhambi hiyo na tunahitaji neema ya Sacramenti ya Ubatizo ili tufutiwe dhambi hiyo. Ndio maana Kristu alitoa amri kwa wafuasi wake watangaze injili na kubatiza watu wote katika kanuni ya Utatu Mtakatifu (Mathayo 28:19). Japo Mama alipewa neema kamili, kamwe hakuondolewa uhuru wa nafsi yake anayopewa kila binadamu ya kuchagua jema ama baya yaani free will. Wanaopinga fundisho hili la imani wakumbuke kuwa Mungu ni muweza wa yote, aliumba kila kitu na kuona ni chema (Mwanzo 1:31) Hivyo Adam na ubavu wake (Eva) waliumbwa wema bila doa la dhambi. Dhambi ilikua haijaingia duniani, hivo kama ilivo kwa Maria, Adam aliumbwa safi (Immaculate). Iweje tena Mungu ashindwe mfanyia mwanamke aliyebarikiwa kuliko wanawake wote? (luka 1:42) Kuliko hata Eva, ambaye naye aliumbwa bila dhambi ya asili? Lakini hata hivo Mungu hakumuondolea Adam zawadi yake ya nafsi kuwa huru katika kuchagua. Adam kupitia Eva akachagua baya na dhambi ikaingia duniani kwa kupitia kwake. Hivyo kila mzaliwa wa Adam anarithi dhambi hiyo ya asili na kwa ajili ya dhambi moja kifo kikaingia duniani (Warumi 5:12).  Ndio maana Kristu akamwambia Nikodemu Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu”(Yohana 3:5)




Je, kama Mama Maria amekingiwa dhambi ya asili toka milele, wapi tunapata habari hizo katika Biblia?

Turejee kitabu cha Mwanzo ambapo Mungu anamwelezea mwovu shetani jinsi atakavyo ikomboa dunia. Anasema nitafanya Uadui kati yako na mwanamke, mbegu yake itakanyaga kichwa chako (Mwanzo 3:15). Katika kutafsiri mstari huu, Kanisa na Mababa wa Kanisa wanatafakari, Je, mbegu hiyo ni ipi (Nani) atakaye mkanyaga shetani?  Wakristu wote tunaafiki na kukiri pamoja na Kanisa kuwa mbegu hiyo (huyo) ni Kristu mbarikiwa. Kwa kifo na ufufuko wake ameshinda mauti na kumkanyaga shetani. Hivyo yeye ndiye mbegu. Na kamwe Kristu kwa kuwa hakuwa na dhambi hata kidogo (1 Yohana 3:5) hawezi kutoka kwenye mbegu yenye dhambi. Bali yampasa kutoka kwenye mbegu safi. Hivyo huyo mwanamke Mungu aliyemtaja ni Mama Maria na si Eva. Kwani mbegu ya Eva na Adam ni sisi binadamu wote na kwa dhambi ya mtu mmoja (Adam) kifo kikaingia kwetu wote. Lakini Mababa wa Kanisa wakaendelea kutafakari neno "Nitafanya uadui….". Mungu kwa Neema yake anatengeneza “Uadui " kati ya Maria na Shetani. Jambo hili limefanyika miaka karne nyingi kabla hata ya kuzaliwa Maria. Neno uadui ni kukosa mapatanisho na kutoelewana. Tunatengeneza uadui na Mungu pale tunapo tenda dhambi. Pia tunatengeneza uadui na shetani pale tunapotenda mema. Hivyo kwa Mungu kutengeneza uadui kati ya mwanamke (Maria) na shetani, anampatia Maria neema yake ya pekee ili daima Maria atende mema na milele awe adui wa shetani kwa kukataa kutenda dhambi hata zile ndogo. Kama Maria katika maisha yake duniani angeweza hata mara moja kuwa rafiki wa shetani kwa kutenda hata dhambi ndogo tu,  Je,  tuseme basi Mungu ameshindwa tekeleza ahadi yake juu ya mwanamke huyu? HAIWEZEKANI, kwani imeandikwa Mungu ni muweza wa yote (Mathayo 19:26, Luka 1:37, Marko 10:27 ), pia imeandikwa Bwana hakawii kutimiza ahadi yake (2 Petro 3:9), na  pengine tunakiri Mungu si binadamu kubadilisha mawazo yake (1 Samueli 15:29 )

Tunaelewaje kuhusu Utakaso wa Maria katika Hekalu la Bwana(Luka 2:22), Je mstari huu haupingani na fundisho hili?

“Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Musa, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana”

Mstari huu unazungumzia Maria aliyehitaji kutakaswa Hekaluni baada ya kumzaa mtoto Yesu. Hii ilikua ni sheria ya Torati ya Musa iliyohitaji kila mwanamke baada ya kujifungua, inampasa kujitokeza mbele ya Hekalu la Bwana na kutoa sadaka ili apate kusafishwa dhambi ya uchafu uliotokana na kujifungua. Kama Maria alikua msafi asiye na doa la dhambi mbona ilimpasa pia yeye kusafishwa? Hapa jibu linalotolewa ni sawa na jibu alilotoa Kristu kwa Yohana Mbatizaji wakati Yesu anakuja kubatizwa naye. Ubatizo wa Yohana ulikua ni wa Toba na wa kuondolewa dhambi na kusafishwa. Lakini Yesu asiye na doa la dhambi hakuhitaji ubatizo huo. Pia hakuja kutengua sheria ya Torati, hivyo ili haki itendeke anamwambia Yohana “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka” (Mathayo 3:15). Ni hivyo hivyo ilivyotendeka kwa Maria alipohitaji kusafishwa kutokana na sheria za Torati. Si kusafishwa kwa ajili ya dhambi maana hakua na hata moja. Bali alikubali na kuheshimu sheria ili “haki yote itendeke”

Maria Sanduku Jipya la Agano

Katika kitabu cha agano la kale, kama jinsi Mungu alivopendelea kukaa ndani ya Sanduku la Agano ambalo lilikua takatifu na lenye usafi, vivyo hivyo alipendelea kushuka duniani na kukaa miezi tisa ndani mwa sanduku jipya la agano lililo safi yaani Mama Maria. Hivyo basi ndio maana Kanisa hadi hivi leo kupitia mafundisho ya mababa wa Kanisa na mapokeo ya mitume, Mama Maria anaitwa Sanduku jipya la Agano maana Mungu alikaa tumboni mwake kwa miezi tisa. Mt Luka katika injili yake anatupatia uhusiano huo kwa kuonyesha furaha aliyopata Yohana mbatizaji akiwa tumboni mwa mamaye Elizabeth wakati Maria amekwenda mtembelea. Elizabeth anasema mtoto Yahona alicheza kwa furaha. Vivyo hivo Mfalme Daudi pia alicheza kwa furaha mara tu baada ya kurudishwa Sanduku la agano ambapo ndani yupo Mungu (2 Samueli 6:14)). Elizabeth bila hata kujua habari alizopashwa Maria, anajazwa na Roho Mtakatifu na kumlaki Maria kama Mama wa Bwana ambaye ni Mungu mwenyewe katika nafsi ya pili

Mwisho kabisa Mama Maria mwenyewe amedhihirisha ukweli wa fundisho hili kwetu. Kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, Kanisa huadhimisha sikukuu ya Mama yetu wa Lourdes ambapo tunakumbuka Mama Maria kumtokea Mt Benardetta na kujitambulisha jina kama "Ni mimi niliye kingiwa dhambi ya asili " peleka ujumbe wangu kwa wote kwamba watubu na kusali na kumwamini Yesu Kristu ili waokoke. Maria alimtokea kwa mara ya kwanza Mt. Benardeta mwaka 1858 huko Loudes ufaransa

Je, aheshimike Milele?

Anayekubali mafundisho haya ndiye mshika neno la Mungu katika uhalisia wake. Neno la Mungu linatusihi kumheshimu Mama daima katika vizazi vyote vya kale na vijavyo. Biblia inatuambia kuwa tangu kutungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, inatupasa watu wote kumwita Mama Maria “Mwenye Heri”. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri (Luka 1:48). Biblia kutumia neno “Tangu sasa” inataka kutuonyesha kuwa heshima anayopata Mama Maria hadi hivi leo si ngeni kama ilivyoanza kukataliwa na wakristu wenzetu karne ya 16. Heshima hiyo alipewa “Tangu” kipindi kile cha Kristu. Biblia ya Kiingereza inatumia maneno “All generations will call me blessed”. Maneno “All generations” ikimaanisha kila kizazi cha binadamu toka kipindi cha Kristu, kipindi cha matendo ya Mitume, kipindi tunachoishi kwa sasa na daima kitamheshimu Mama wa Mungu na kumwomba atuombee kwa mwanaye Kristu Mfalme ili tupate wokovu

Maria Mama wa Mungu, utuombee sasa na wakati wa kufa kwetu. AMINA 

4 comments:

  1. Amina ujumbe nimeuelewa tec hongera kwa hili. Nashukuru pia nimeelewa sasa sikukuu somo wa jumuiya yangu Mt. Maria Imakulata

    ReplyDelete
  2. Asanteni sana watumishi wa Mungu kwa ufafanuzi mzuri kabisa wa neno la Mungu. Nimeelewa kuwa nipo sehemu sahihi katika kumuabudu Mungu wangu wa kweli kupitia ukristo.Nawaombea kwa Mungu aendelee kuwatumia Kama chombo chake.

    ReplyDelete