Monday, March 3, 2014

MAPOKEO YA MITUME NA BIBLIA

Kristu akitabiri ujio wa Roho Mtakatifu, aliwaambia Mitume wake, Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote….. atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu (Yoh 16:12-14)

Hivyo katika siku ya Pentecost wakiwa Mitume wako pamoja na Mama Maria na wanawake wengine (Matendo ya Mitume 1:14), Roho Mtakatifu akawashukia na ndio rasmi Kanisa likazaliwa na Roho Mtakatifu akakaa nao milele. (Matendo ya Mitume 2:1-4). Mitume wakapewa jukumu la kufundisha na kusimamia ukweli

Je, ukweli huo umetufikia kwa njia ya maandishi tu yaani Biblia Takatifu peke yake?


Ni lazima kusisitiza kabisa kwamba Biblia ni Neno la Mungu na Mungu ndiye mwandishi wakes. Pia kama Neno, ndani mwake hamna upotovu hata kidogo. Wakatoliki wote inatupasa kuamini na kukubali yote yaliyoandikwa katika Biblia kama ufunuo kutoka kwa Mungu. Lakini wakatoliki tunaamini kuwa Si Biblia peke yake yenye chanzo cha ufunuo wote kamili aliokusudia Kristu. Linaonekana ni jambo la kushangaza sana lakini Biblia yenyewe inakubaliana na huu ukweli kwamba si kila kitu alichotenda na kuagiza Kristu kimeandikwa na karamu yaani kwa njia ya maandishi (Yohana 21:25)

Ni kwa njia gani nyingine basi ufunuo wa Kristu umetufikia?

Historia inaonyesha kwamba Mitume, kama ilivyokuwa kipindi cha Kristu walieneza Injili kwa kuhubiri kwanza kabla ya kuweka Imani katika maandishi. Wote 12 na wale wafuasi 70 walipewa jukumu la kusambaza habari njema. Lakini Biblia yetu inavyo vitabu 27 tu vya agano jipya na kati ya hivyo 12 vimeandikwa na Paulo peke yake. Je, kazi za Mitume wengine zilizokosekana basi zimekosa ukweli? Historia ya Kanisa huzungumzia kuwa katika kitabu cha Agano Jipya, kabla hata ya Injili (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) nne kuandikwa, waraka wa kwanza kuandikwa ulikua ni barua ya kwanza ya Paulo kwa Wakorintho. Baadaye ndio ikaandikwa Injili ya kwanza ya Marko aliyekua mwanafunzi wa Mtume Petro. Kama mwanafunzi wa Petro, Marko hakushuhudia kwa macho uwepo wa Yesu duniani bali alipewa ufunuo huo na Petro mwenyewe kwa njia ya mafundisho na si kwa maandishi. Ndipo basi ikaandikwa Injili ya Marko ambayo ni ya kwanza kabisa katika Injili nne. Japo katika list ya Injili imewekwa namba 2 katika Biblia. Baada ya Marko ndipo zikaandikwa Injili nyingine za Matayo, luka na mwisho Yohana. Pia zikafuata nyaraka mbali mbali za mitume kama tunavyozishuhudia katika agano jipya. Ifamike kwa undani kabisa kwamba zilikuwako Injili nyingi mno zaidi ya hizo nne, pia ziliandikwa nyaraka mbali mbali nyingi zaidi ya zile tunazofahamu kwenye Biblia. Yasemekama kwa jumla kulikua na nyaraka na vitabu zaidi ya 80. Kumbe Agano jipya lenye vitabu 27 tu vya ukweli vilichaguliwa katika ya vingi sana vilivyokuwa vimeandikwa lakini vya kupotosha Imani. Hapo ndipo unapatikana umuhimu wa kutenganisha neno la Mungu na maandishi ya vitabu. Kanisa liliamua neno la Mungu linapatikana katika vitabu 27 tu vya agano jipya pamoja na vile vya agano la kale. Ni Kanisa (Katoliki la Mitume) lililo amnua juu ya Idadi ya vitabu vya Biblia kwa mara ya kwanza mnamo Karne ya nne mwaka 393 katika mtaguso wa Hippo. Idadi hiyo ya vitabu ndiyo itumikayo mpaka sasa. Twaweza jiuliza, Je, Biblia tuliyonayo ndiyo yenyewe iliyomua idadi ya vitabu? HAPANA, maana kama kitabu kamili na mkusanyiko wa Injili na Nyaraka bado hakikuweko. Je, paliwahi kutokea Malaika aliyetumwa kutoa Idadi ya vitabu?  HAPANA, Je ilikua ni kazi ya Roho Mtakatifu kupitia Kanisa Katoliki na mababa wa Kanisa? NDIYO. Lakini hili liliwezekana vipi?  Ndicho tunachojaribu kuelezea hapa

 Historia inaonyesha kuwa kulitokea machafuko makubwa nchini Israel mwaka 70 baada ya Kristu. Hizi zilikua ni jitihada za wayahudi kuleta mapinduzi juu ya utawala wa Roma nchini mwao.Machafuko haya yalitabiriwa na Kristu katika Injiliya Matayo alipozungumizia kuanguka kwa Hekalu na kutoa amri kwa wafuasi wake yaani wakristu kukimbia mara tu machafuko haya yatakapo anza kutokea (Matayo 24:15-21)


Hivyo Kanisa na wakristu Israeli wakasambaratika na kuzidiwa nguvu. Wakristu wengi walikimbia nchi. Kwa upande mwingine Kanisa la Roma lililoanzishwa na Mitume Petro na Paulo (ambao pia wote walikufa mjini Roma), japo dogo na changa likasimama kama Kanisa Mama na Askofu wake kupewa nafasi ya kwanza kiheshima na mamlaka ya kuhakikisha umoja katika makanisa. Kanisa hili la Roma lilijengwa juu ya miamba Petro na Paulo na ile imani ya kitume ikasimama imara. Ikumbukwe pia kuwa si Kanisa la Roma tu lililo simama katika imani ya mitume yaani Apostolic, bali kuna Kanisa la Mashariki Constantinopo wakristu wa Orthodox. Hili lilianzishwa na Askofu wake Mtume Andrea kaka yake Mtume Petro. Pia kanisa la Kitume la Alexandria Misri wakristu Oriento orthodox. Hili lilianzishwa na Askofu Marko (mwandishi wa Injili) pia na mwanafunzi wa Petro. Pia kanisa la mashariki Syria wakristu Nestorian. Pia Kanisa la kitume la India lililoanzishwa na Mtume Tomaso. Pamoja na Kanisa la Orthodox Ethiopia lililosimamiwa na Kanisa la Oriento Misri. Makanisa haya hadi hivi leo yapo na yanayo mapokeo kamili ya mitume. Lakini lenye heshima kuu ni kanisa la Roma lililoanzishwa juu ya miamba Petro na Paulo. Ni kwa kupitia imani ya mapokeo ndiyo Kanisa likaweza kuamua juu ya idadi ya vitabu vya Biblia. Hivyo imani hiyo ya mapokeo yaani Tradition ndiyo iliyotumika kuhakiki na kuchagua vitabu. Bila imani hiyo mpaka hivi leo wakristu tungebaki na changamoto ya kujua ni vitabu vipi vya ukweli na vipi ni vya kupotosha.

Je, Mapokeo ya Mitume ni nini (Tradition)
Katika kueneza Injili basi mitume wa Yesu walihubiri kwa maneno na barua huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Ni hapo basi ndipo tunapokutana na neno la Mungu lililohubiriwa (Tradition) lakini halikuwekwa katika maandishi (written scripture yaani Biblia)
Hili neno la Mungu la mahubiri tu ndilo tuitalo Mapokeo ya Mitume. Katika kuhakikisha imani ya mapokeo inasambazwa na kulindwa, Mitume hao 12 walianzisha makanisa mbali mbali na kuchagua viongozi yaani Maaskofu kwa kwa njia ya kuwawekea mikono wafuasi wao (1 Timoteo 4:14) na kuwafanya maaskofu. Ilipohitajika walikuza na kuimarisha imani ya viongozi hao kwa  kuwaandikia barua na nyaraka mbali mbali ambazo ndizo zimekusanywa na Kanisa na kufanywa Biblia. Kanisa lililo jengwa juu ya mwamba Petro (Matayo 16:18) ndilo liliachiwa mamlaka ya kulinda na kutafsiri Injili ya Bwana kwa maana Kanisa ni nguzo na msingi wa kweli(1 Timotheo 3:15). Kweli tuliyoipokea kwa njia hizo mbili zilizo sawa katika mamlaka kwa maana zote ni neno kutoka kwa Bwana. Kanisa hilo la mitume japo ni moja (Catholic) lakini limegawanyika katika makanisa mengi mengi lakini yenye imani sawa ya Mitume (Roma, Orthodox, Oriental orthodox, Nestorian) mpaka hivi leo linafundisha na kushikilia imani hiyo ya mitume mapokeo (Tradition) na Biblia. Ichukuliwe tahadhari kubwa ya kushawishika kutafsiri neno “Tradition” kama “tradition” yaani tamaduni. Makanisa haya yanaposema Tradition hutumia herufi kubwa “T” kukwepa tafsiri ya herufi ndogo “t” inayomaanisha tamaduni na desturi za binadamu zinazobadilika. Maana halisi ya neon Tradition ni “Mapokeo” na si ya binadamu bali ya Mitume katika ufunuo wa Roho Mtakatifu. Imani hii kamwe haibadiriki. Kwa sikitiko kubwa sana fundisho hili la mapokeo lilipingwa na kukataliwa kwa mara ya kwanza kabisa mnamo karne ya 15 na wakristu wenzetu wa Protestanti. Hii ikasababisha mgawanyiko mkubwa sana wa Kanisa hadi hivi leo huku waprotestanti wakiamini kuwa ni Biblia peke yake tu ndiyo chanzo cha ufunuo kamili. Je, Biblia yenyewe imefundisha mtazamo huu? HAPANA.. kama tulivyoona hapo mwanzo, Biblia yenyewe inakiri kuwa si yote aliyotenda na kusema Yesu yameandikwa katika Biblia (Yohana 21:25). Mengine hayapo. Pia Mt Paulo katika waraka wake kwa Wathesalonike anatenganisha nia hizi mbili na kuwasihi kwamba “….ndugu wapendwa, simameni imara na mshike sana yale mafundisho tuliyowapeni katika mahubiri yetu na kwa barua zetu (2 Wathesalonike 2:15)”. Pia katika matendo ya mitume Mt. Paulo anatamka maneno ya Yesu ambayo hayapatikani kabisa katika Injili za Biblia akiwaambia wazee wa Kanisa la Efeso akiwasihi kwamba Yesu alisema “ Kuna Baraka kubwa zaidi katika kutoa kuliko kupokea (Matendo ya Mitume 20:35). Kama maneno haya hayapatikani katika Injili basi ni dhahiri kabisa Paulo aliyapata katika Mapokeo yaliyoletwa na Roho Mtakatifu. Mfano mwingine ni katika waraka wa Mt. Yuda akiongelea ushindani kati ya Malaika Mikaeli na shetani juu ya mwili wa Musa (Yuda 1:9). Tukio hili ambalo halikuandikwa mahala popote katika agano la kale lakini Yuda alililipata kwa njia ya mapokeo. Inapatikana mifano mingi tu ya kulinda hoja hii ya ukweli katika Biblia.

Ifuatayo ni mifano ya mapokeo ya Kanisa Katoliki la Mitume ambayo haijawekwa kinagaubaga katika biblia. Ni vyema kuuliza, Je Biblia imekataza mapokeao haya? HAPANA, bali Biblia inayo mifano mingi inayotetea mapokeo haya kama tutakavyoona hapo baadaye tutakapo tembelea na kuelezea kwa undani kila moja ya mapokeo haya. Yafuatayo ni mapokeo 

1. Mafundisho yote ya Kanisa kuhusu Mama Maria
1.1  Alizaliwa bila dhambi ya asili hivyo hakua na doa la dhambi (Immaculate Conception)
1.2  Baada ya kumzaa Kristu alibaki Bikira milele (Perpetual Virginity)
1.3  Baada kumaliza mda wake alipalizwa mbinnguni mwili na roho (Bodily Assumption)
1.4  Anatuombea sisi wakosefu
2. Utatu Mtakatifu (Trinity)
3. Kuombea roho za marehemu (Pray for the dead and communion of Saints)
4. Toharani (Purgatory)
5. Kuwaheshimu Watakatifu, Malaika na kuomba maombezi yao (Veneration and Intercession of Saints)
6. Kuheshimu Mabaki ya Watakatifu (Veneration of Relics)
7. Kuheshimu (kamwe c kuabudu) picha na sanamu (Holy Icon & Statue veneration)
8. Ubatizo wa watoto wachanga (Infant Baptism)
9. Mtazamo wa Misa kama Sadaka ya Kristu (Mass as a Sacrifice)
10. Mitaguso ya kiukumeni (Ecumenical Councils)

Tutapata muda wa kuangalia kwa undani mafundisho haya moja baada ya nyingine

1 comment: