Wednesday, January 2, 2013

MIMBARI ZILIZOSIMAMISHWA NA MAENDELEO YA KISASA


“Kama Mt. Paulo angeishi leo”, anasema Mwenyeheri Giacomo Alberione, mwanzilishi wa watawa wa Mtakatifu Paulo, “angefanya bidii ya kutumia mimbari za juu zaidi zilizosimamishwa na maendeleo ya kisasa: uchapishaji, sinema, redio, televisheni”. Wakati Mwenyeheri Giacomo akisema hayo, na mpaka mauti ilipomfika, ulimwengu ulikuwa bado haujajizamisha katika matumizi ya mawasiliano ya kisasa zaidi kama intaneti. Mwenyeheri Alberione amefariki mwaka 1971 wakati mapinduzi ya mtandao yameshika kasi miaka ya 90 baada ya mwanasayansi Tim Berners-Lee wa Uingereza kugundua matumizi ya mtandao mnamo mwaka 1989 kwa namna tunayokuwa nayo leo.

Katika ulimwengu wa kisasa, njia za mawasiliano ya jamii: magazeti, televisheni, radio, intaneti n.k, zinabaki kuwa “mfereji” mpana, wenye nguvu na wenye uwezo wa ajabu katika kufikisha ujumbe na kushawishi mwelekeo wa jamii karibu juu ya kila jambo. Mfereji huu pia umethibitisha kuwa na uwezo wa kupitisha “maji masafi” na hata “maji machafu” pia.

Intaneti, kama ilivyo kwa kila jambo na kila kitu, katika yenyewe haina tatizo. “ Hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake” (Rum. 14:14). Uzuri au ubaya wa kila jambo unajidhihirisha katika matumizi. Mwanadamu kupitia paji la akili, mang’amuzi na ubunifu anaweza kuendeleza kazi ya uumbaji au kuiharibu. Njia za mawasiliano ya kijamii zinapewa sura na mwanadamu pale anapozitumia katika kufikisha ujumbe kwa jamii

Mwanadamu anaweza, katika kuzitumia njia hizi, akaifikishia jamii sura ya kutisha na kukatisha tamaa au sura ya matumaini na yenye kuweza kurahisisha ujenzi wa dhamiri ya jamii. Lakini hata pale inapotokea kuwa njia na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinawasilisha sura isiyopendeza kwa kufikisha ujumbe usio sahihi na wa kubomoa badala ya kujenga, hatupaswi kuvikimbia. Kwa sababu hii ni njia, na hivi ni vyombo visivyoepukika vya mawasiliano ya haraka. Ni umuhimu huu ndiyo unaotufanya kuvitumia ili kuonesha upande mwingine, yaani jinsi vyombo hivi vinavyoweza kutumika kujenga na kuielimisha jamii.

Tusipovitumia vyombo vya mawasiliano ya kijamii kupitishia “maji safi”, wale wanaoutumia kupitishia “maji machafu” wanazidi kudhihirishia kuwa hawana muda wa kupoteza na kubweteka. Wako kazini! Na hiyo ndio kazi yao na lengo lao!

Tusipoutumia mfereji huu kupitishia “maji safi” tutakuwa pia tunawanyima fursa wale wote ambao wangependa kuangalia kwa makini pande mbili za sarafu, tena kwa haraka kupitia njia hii ya mawasiliano. Zaidi sana tutakuwa tunawanyima wale wote ambao wanatumia vyombo vya njia za mawasiliano kupata fursa mbadala inayoweza kuwasaidia kujua, kupima, kulinganisha lipi ni sahihi na lipi si sahihi na kisha kuchagua ni njia ipi wafuate wakiongozwa na uhuru wa utashi na dhamiri zao

Kanisa linavipa vyombo vya mawasiliano ya jamii umuhimu mkubwa. Hii ni kwa sababu vina nafasi muhimu katika uinjilishaji. Zaidi ya hayo, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinawasaidia waamini kupata habari mbalimbali juu na hata dhidi ya imani  yao jambo linalowasaidia kukomaa katika safari yao ya imani.

Kanisa la karne za mwanzo lilijikuta pia likikabiliwa na changamoto za wakati wake, nyingi zikifanana karibu na hizi za nyakati zetu, hususani katika hitaji la kukuza uwezo wa kupambanua na kuchagua jambo lipi ni la kweli na sahihi katika elimu na mtaala wa ulimwengu wa “kipagani”. Ikumbukwe kuwa wakati wa kipindi cha Kanisa la mwanzo na hasa wakati wa kipindi cha Mababa wa Kanisa wa karne ya nne na ya tano, mtaala wa elimu ya wakati huo ulikuwa ule wa shule za “kipagani”. Katika shule hizi walisoma wapagani na wakristo pia. Kazi za fasihi ziliyosomwa mashuleni zilikuwa ni za “kipagani”. Kazi za fasihi, historia na falsafa zilizotumika wakati huo zilikuwa zile za elimu ya kilatini na kiyunani (classical), za akina Homer, Tucidide, Cicero, Virgil, Plato, Aristotle n.k.  Waalimu maarufu wa kipagani kama Libanio ndio waliowafundisha Mababa wa Kanisa maarufu kama Yohane Krisostom.  

Msisitizo wa Kanisa la wakati huo ulikuwa ni juu ya katekesi ya imani na umakini wa wanafunzi wakristo katika kuweza kupambanua yale wanayojifunza shuleni. Mababa wa Kanisa ambao walikuwa ni “makatekista” mashuhuri waliwasisitizia wanafunzi wakristo kujifunza kuchuja yale waliyojifunza shule kwa mwanga wa imani yao

Mt. Basili Mkuu, kwa mfano, katika hotuba yake  kwa vijana anasema: Kwa upande wetu, ni lazima tuhudhurie mihadhara hii tukiiga mfano wa nyuki. Nyuki hawatui juu ya kila ua pasipo kuchagua, na hata juu ya maua yale ambayo juu yake wanatua hawachukui kila kitu, wanapokuwa tayari wamechukua kile kinachofaa, wanaacha kile kisichofaa: hata sisi, kama tuna hekima, tukishachukua kutoka kwao (waandishi wapagani) kile kinachotufaa, na kinachopatana na ukweli, tunaacha makombo ( Hotuba kwa vijana, 4).

Kimsingi, Mababa wa Kanisa waling’amua kuwa si kila kilichomo katika mafundisho ya kipagani ni ubatili. Waling’amua kuwa ilikuwamo hekima pia katika mafundisho hayo. Ndiyo maana, Kanisa halikuacha kutoa elimu ya falsafa ya Wayunani kwa sababu liliamini kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kuweza kufikisha ujumbe wake kwa jamii ya wasomi wa wakati huo. Mt. Justino (c. 100-165) anasema, kama Agano la Kale linatuelekeza kwa Kristo kama jinsi taswira inavyotuelekeza kwenye uhalisia inaouwakilisha, basi falsafa ya kiyunani nayo inatuelekeza  kwa Kristo na Injili, kama jinsi sehemu ya kitu isivyokamilika bila kuungana na kitu kizima. Kadiri ya Mt Justino , Agano la Kale na falsafa ya kiyunani ni njia mbili zinazotuelekeza kwa Kristo.

Umuhimu wa kuwasilisha na kufafanua imani yetu na mafundisho ya Kanisa ndio inayotuvuta kuingia ulingoni ili nasi tuweze kutoa mchango watu, hata kama ni mdogo, kupitia “mimbari” hii ya kisasa.

Amepata kuandika Svetonio, mwanahistoria wa kirumi (c. 69-122) juu ya Kaisari Tito Flavio aliyetawala kati ya mwaka 79-81 BK (Tito alikuwa  moja ya makaisari wa Kirumi walioheshimiwa na kupendwa sana)   akisema kuwa Tito alijiwekwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa siku haipiti bila kutenda tendo jema lenye kuleta faraja na matumaini kwa yeyote anayemwendea.  Siku moja akiwa mezani wakati wa chakula cha jioni, Tito aligundua kuwa siku hiyo ilipita na hakuwa amefanya tendo lolote jema. Ghafla alipaaza sauti akasema: “Amici, diem perdidi!” Rafiki zangu, nimepoteza siku! Tusingependa nasi kupoteza fursa ya kutumia mimbari hii ya teknolojia ya kisasa.

Na Fr. Ray Saba



No comments:

Post a Comment