“Kama
Mt. Paulo angeishi leo”, anasema Mwenyeheri Giacomo Alberione, mwanzilishi wa
watawa wa Mtakatifu Paulo, “angefanya bidii ya kutumia mimbari za juu zaidi
zilizosimamishwa na maendeleo ya kisasa: uchapishaji, sinema, redio,
televisheni”. Wakati Mwenyeheri Giacomo akisema hayo, na mpaka mauti
ilipomfika, ulimwengu ulikuwa bado haujajizamisha katika matumizi ya mawasiliano
ya kisasa zaidi kama intaneti. Mwenyeheri Alberione amefariki mwaka 1971 wakati
mapinduzi ya mtandao yameshika kasi miaka ya 90 baada ya mwanasayansi Tim
Berners-Lee wa Uingereza kugundua matumizi ya mtandao mnamo mwaka 1989 kwa
namna tunayokuwa nayo leo.
Katika
ulimwengu wa kisasa, njia za mawasiliano ya jamii: magazeti, televisheni,
radio, intaneti n.k, zinabaki kuwa “mfereji” mpana, wenye nguvu na wenye uwezo
wa ajabu katika kufikisha ujumbe na kushawishi mwelekeo wa jamii karibu juu ya
kila jambo. Mfereji huu pia umethibitisha kuwa na uwezo wa kupitisha “maji
masafi” na hata “maji machafu” pia.
Intaneti, kama ilivyo
kwa kila jambo na kila kitu, katika yenyewe haina tatizo. “ Hakuna kitu kilicho
najisi kwa asili yake” (Rum. 14:14). Uzuri au ubaya wa kila jambo
unajidhihirisha katika matumizi. Mwanadamu kupitia paji la akili, mang’amuzi na
ubunifu anaweza kuendeleza kazi ya uumbaji au kuiharibu. Njia za mawasiliano ya
kijamii zinapewa sura na mwanadamu pale anapozitumia katika kufikisha ujumbe
kwa jamii
Mwanadamu anaweza,
katika kuzitumia njia hizi, akaifikishia jamii sura ya kutisha na kukatisha
tamaa au sura ya matumaini na yenye kuweza kurahisisha ujenzi wa dhamiri ya
jamii. Lakini hata pale inapotokea kuwa njia na vyombo vya mawasiliano ya jamii
vinawasilisha sura isiyopendeza kwa kufikisha ujumbe usio sahihi na wa kubomoa
badala ya kujenga, hatupaswi kuvikimbia. Kwa sababu hii ni njia, na hivi ni
vyombo visivyoepukika vya mawasiliano ya haraka. Ni umuhimu huu ndiyo
unaotufanya kuvitumia ili kuonesha upande mwingine, yaani jinsi vyombo hivi
vinavyoweza kutumika kujenga na kuielimisha jamii.
Tusipovitumia
vyombo vya mawasiliano ya kijamii kupitishia “maji safi”, wale wanaoutumia
kupitishia “maji machafu” wanazidi kudhihirishia kuwa hawana muda wa kupoteza
na kubweteka. Wako kazini! Na hiyo ndio kazi yao na lengo lao!
Tusipoutumia mfereji huu kupitishia “maji safi” tutakuwa pia
tunawanyima fursa wale wote ambao wangependa kuangalia kwa makini pande mbili
za sarafu, tena kwa haraka kupitia njia hii ya mawasiliano. Zaidi sana tutakuwa
tunawanyima wale wote ambao wanatumia vyombo vya njia za mawasiliano kupata fursa
mbadala inayoweza kuwasaidia kujua, kupima, kulinganisha lipi ni sahihi na lipi
si sahihi na kisha kuchagua ni njia ipi wafuate wakiongozwa na uhuru wa utashi
na dhamiri zao
Kanisa
linavipa vyombo vya mawasiliano ya jamii umuhimu mkubwa. Hii ni kwa sababu vina
nafasi muhimu katika uinjilishaji. Zaidi ya hayo, vyombo vya mawasiliano ya
jamii vinawasaidia waamini kupata habari mbalimbali juu na hata dhidi ya
imani yao jambo linalowasaidia kukomaa
katika safari yao ya imani.
Kanisa
la karne za mwanzo lilijikuta pia likikabiliwa na changamoto za wakati wake,
nyingi zikifanana karibu na hizi za nyakati zetu, hususani katika hitaji la
kukuza uwezo wa kupambanua na kuchagua jambo lipi ni la kweli na sahihi katika
elimu na mtaala wa ulimwengu wa “kipagani”. Ikumbukwe kuwa wakati wa kipindi
cha Kanisa la mwanzo na hasa wakati wa kipindi cha Mababa wa Kanisa wa karne ya
nne na ya tano, mtaala wa elimu ya wakati huo ulikuwa ule wa shule za
“kipagani”. Katika shule hizi walisoma wapagani na wakristo pia. Kazi za fasihi
ziliyosomwa mashuleni zilikuwa ni za “kipagani”. Kazi za fasihi, historia na
falsafa zilizotumika wakati huo zilikuwa zile za elimu ya kilatini na kiyunani
(classical), za akina Homer, Tucidide, Cicero,
Virgil, Plato, Aristotle n.k. Waalimu
maarufu wa kipagani kama Libanio ndio waliowafundisha Mababa wa Kanisa maarufu kama Yohane Krisostom.
Msisitizo
wa Kanisa la wakati huo ulikuwa ni juu ya katekesi ya imani na umakini wa
wanafunzi wakristo katika kuweza kupambanua yale wanayojifunza shuleni. Mababa
wa Kanisa ambao walikuwa ni “makatekista” mashuhuri waliwasisitizia wanafunzi
wakristo kujifunza kuchuja yale waliyojifunza shule kwa mwanga wa imani yao.
Mt.
Basili Mkuu, kwa mfano, katika hotuba yake kwa vijana anasema: Kwa upande wetu, ni lazima
tuhudhurie mihadhara hii tukiiga mfano wa nyuki. Nyuki hawatui juu ya kila ua
pasipo kuchagua, na hata juu ya maua yale ambayo juu yake wanatua hawachukui
kila kitu, wanapokuwa tayari wamechukua kile kinachofaa, wanaacha kile
kisichofaa: hata sisi, kama tuna hekima, tukishachukua kutoka kwao (waandishi
wapagani) kile kinachotufaa, na kinachopatana na ukweli, tunaacha makombo ( Hotuba kwa vijana, 4).
Kimsingi,
Mababa wa Kanisa waling’amua kuwa si kila kilichomo katika mafundisho ya
kipagani ni ubatili. Waling’amua kuwa ilikuwamo hekima pia katika mafundisho
hayo. Ndiyo maana, Kanisa halikuacha kutoa elimu ya falsafa ya Wayunani kwa
sababu liliamini kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kuweza kufikisha ujumbe wake kwa
jamii ya wasomi wa wakati huo. Mt. Justino (c. 100-165) anasema, kama Agano la Kale linatuelekeza kwa Kristo
kama jinsi taswira inavyotuelekeza kwenye uhalisia inaouwakilisha, basi falsafa
ya kiyunani nayo inatuelekeza kwa Kristo
na Injili, kama jinsi sehemu ya kitu isivyokamilika bila kuungana na kitu
kizima. Kadiri ya Mt Justino , Agano la
Kale na falsafa ya kiyunani ni njia mbili zinazotuelekeza kwa
Kristo.
Umuhimu wa
kuwasilisha na kufafanua imani yetu na mafundisho ya Kanisa ndio inayotuvuta
kuingia ulingoni ili nasi tuweze kutoa mchango watu, hata kama ni mdogo,
kupitia “mimbari” hii ya kisasa.
Amepata
kuandika Svetonio, mwanahistoria wa kirumi (c. 69-122) juu ya Kaisari Tito
Flavio aliyetawala kati ya mwaka 79-81 BK (Tito alikuwa moja ya makaisari wa Kirumi walioheshimiwa na
kupendwa sana) akisema kuwa Tito
alijiwekwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa siku haipiti bila kutenda tendo jema
lenye kuleta faraja na matumaini kwa yeyote anayemwendea. Siku moja akiwa mezani wakati wa chakula cha
jioni, Tito aligundua kuwa siku hiyo ilipita na hakuwa amefanya tendo lolote
jema. Ghafla alipaaza sauti akasema: “Amici,
diem perdidi!” Rafiki zangu, nimepoteza siku! Tusingependa nasi kupoteza
fursa ya kutumia mimbari hii ya teknolojia ya kisasa.