Mafundisho ya Kanisa
kuhusu Mama Maria kamwe si mageni bali yalisimamiwa na Kanisa na wakristu wote toka
karne ya kwanza baada ya Kristu. Itakua ni vyema kutoa kwa ufupi historia ya
fundisho hilo linalomhusu Mama Maria. Kanisa linafundisha kuwa katika kipindi
chote cha maisha yake duniani, Mama Maria kwa neema za Mungu hakutenda dhambi wala
hakua na doa la dhambi. Kanisa hilo Moja la mitume la Mashariki (Orthodox) na
Magharibi (Roma Katoliki) hata baada ya kuvunjika umoja wao mnamo mwaka 1054
karne ya 11, bado linafundisha na kushikilia imani hiyo mpake sasa. Kwa huzuni kubwa
Kanisa la magharibi (Roma Katoliki) pia likavunjika karne ya 16 na kutengeneza
pande mbili za Waprotestanti na Wakatoliki huku baadhi ya Waprotestanti
wakikataa fundisho hilo japo si wote kama ilivyobaki kwa Martin Luther ambaye hakuonyesha
kupinga. Heshima aliyokuwa akipewa Mama ikapuuziwa na msaada wake wa kutuombea
na kuturudisha kwa mwanaye Kristu ukakataliwa na baadhi ya wakristu. Hivyo basi Kanisa la magharibi
likaendelea kugawanyika katika mafundisho yake. Ili wakatoliki wasitetereke
katika imani yao juu ya Mama Maria, mnamo mwaka 1854 Baba Mtakatifu Pius IX
(Mwenye Heri) kama mrithi wa kiti cha Mtume Petro, kupitia mamlaka aliyopewa ya
kufunga na kufungua (Mathayo 16:19) akatangaza kupitia heshima ya kiti hicho
yaani ex cathedra fundisho la imani
yaani Dogma ambalo humpasa kila mkatoliki kuamini bila kupinga kwa
kuwa dogma ni fundisho la Roho Mtakatifu mwenyewe. Hivyo kama Dogma, Mama Maria akatangazwa kuzaliwa
bila dhambi ya asili yaani Immaculate Conception. Neno
Imakulata (immaculate) maana yake ni usafi usio na doa la uchafu.
Iliwezekana vipi Mama Maria kukingiwa dhambi ya asili na
kuishi bila dhambi?
Injili ya Luka inatuambia kuwa
malaika Gabrieli anamsalimu Mama Maria kwa salamu ya pekee kabisa akisema
"Salamu Maria umejaa Neema, Bwana yu
nawe" (luka 1:28). Neema basi ni kitu gani? Neema ni zawadi ya bure
itokayo kwa Mungu Baba, zawadi hii kwa mafundisho ya Mtume Paulo ndiyo
ituokoayo (Waefeso 2). Hakuna binadamu kwa matendo yake mwenyewe anaweza
kuokolewa bila Neema ya Mungu. Tukiendelea kutafakari salamu ya malaika Gabriel,
tunakutana na neno "umejaa neema".
Neno kujaa linaashiria kipimo kamili kabisa kisichokua na upungufu hata kidogo.
Hivyo Mama Maria alijazwa Neema ya pekee kuliko ya mtu yeyote yule. Neema hiyo
ndiyo iliyomfanya aweze kushinda majaribu yake yote. Lakini Je, jambo hili
ameweza kulifanya kwa nguvu zake mwenyewe. HAPANA, Mama Maria alifahamu kwamba
naye aliokolewa kwa kukingiwa dhambi hivyo anasema katika mwimbo wake "Magnificat
" akisema “Na roho yangu inamfurahia
Mungu Mwokozi wangu” (Luka 1:47). Neema itokayo kwa Bwana ndio iokoayo.
Mama Maria ni binadamu na ni kiumbe cha Mungu kama sisi wote tulivyo. Lakini
kwa ule utayari wake katika kushiriki ule mpango wa Mungu wa kuikomboa Dunia
kwa kukubali kwa hiari na kusema NDIYO (..Na
iwe kwangu kama ulivyosema (Luka 1:38) na kwa neema tele za Kristu mwanaye,
basi Mungu toka milele alimpatia Maria neema hiyo kabla hata hajamuumba. Ndipo
wanakoliki tunapokiri kwamba Mama alikingiwa dhambi ya asili kabla hata ya
kuumbwa yaani Immaculate Conception. Japo Maria ni binadamu kamili kama sisi,
tofauti ni kuwa sisi tunazaliwa na dhambi hiyo na tunahitaji neema ya
Sacramenti ya Ubatizo ili tufutiwe dhambi hiyo. Ndio maana Kristu alitoa amri
kwa wafuasi wake watangaze injili na kubatiza watu wote katika kanuni ya Utatu
Mtakatifu (Mathayo 28:19). Japo Mama alipewa neema kamili, kamwe hakuondolewa
uhuru wa nafsi yake anayopewa kila binadamu ya kuchagua jema ama baya yaani free
will. Wanaopinga fundisho hili la imani wakumbuke kuwa Mungu ni muweza wa yote,
aliumba kila kitu na kuona ni chema (Mwanzo 1:31) Hivyo Adam na ubavu wake (Eva)
waliumbwa wema bila doa la dhambi. Dhambi ilikua haijaingia duniani, hivo kama
ilivo kwa Maria, Adam aliumbwa safi (Immaculate). Iweje tena Mungu ashindwe
mfanyia mwanamke aliyebarikiwa kuliko wanawake wote? (luka 1:42) Kuliko hata
Eva, ambaye naye aliumbwa bila dhambi ya asili? Lakini hata hivo Mungu
hakumuondolea Adam zawadi yake ya nafsi kuwa huru katika kuchagua. Adam kupitia
Eva akachagua baya na dhambi ikaingia duniani kwa kupitia kwake. Hivyo kila
mzaliwa wa Adam anarithi dhambi hiyo ya asili na kwa ajili ya dhambi moja kifo
kikaingia duniani (Warumi 5:12). Ndio
maana Kristu akamwambia Nikodemu “Kweli
nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme
wa Mungu”(Yohana 3:5)
Je, kama Mama Maria amekingiwa dhambi ya asili toka milele,
wapi tunapata habari hizo katika Biblia?
Turejee kitabu cha Mwanzo ambapo Mungu
anamwelezea mwovu shetani jinsi atakavyo ikomboa dunia. Anasema nitafanya Uadui kati yako na mwanamke, mbegu
yake itakanyaga kichwa chako (Mwanzo 3:15). Katika kutafsiri mstari huu,
Kanisa na Mababa wa Kanisa wanatafakari, Je, mbegu hiyo ni ipi (Nani) atakaye
mkanyaga shetani? Wakristu wote tunaafiki na kukiri pamoja na Kanisa
kuwa mbegu hiyo (huyo) ni Kristu mbarikiwa. Kwa kifo na ufufuko wake ameshinda
mauti na kumkanyaga shetani. Hivyo yeye ndiye mbegu. Na kamwe Kristu kwa kuwa
hakuwa na dhambi hata kidogo (1 Yohana 3:5) hawezi kutoka kwenye mbegu
yenye dhambi. Bali yampasa kutoka kwenye mbegu safi. Hivyo huyo mwanamke Mungu
aliyemtaja ni Mama Maria na si Eva. Kwani mbegu ya Eva na Adam ni sisi binadamu
wote na kwa dhambi ya mtu mmoja (Adam) kifo kikaingia kwetu wote. Lakini Mababa
wa Kanisa wakaendelea kutafakari neno "Nitafanya
uadui….". Mungu kwa Neema yake anatengeneza “Uadui " kati ya Maria na Shetani. Jambo hili limefanyika miaka
karne nyingi kabla hata ya kuzaliwa Maria. Neno uadui ni kukosa mapatanisho na
kutoelewana. Tunatengeneza uadui na Mungu pale tunapo tenda dhambi. Pia
tunatengeneza uadui na shetani pale tunapotenda mema. Hivyo kwa Mungu
kutengeneza uadui kati ya mwanamke (Maria) na shetani, anampatia Maria neema
yake ya pekee ili daima Maria atende mema na milele awe adui wa shetani kwa kukataa
kutenda dhambi hata zile ndogo. Kama Maria katika maisha yake duniani angeweza
hata mara moja kuwa rafiki wa shetani kwa kutenda hata dhambi ndogo
tu, Je, tuseme basi Mungu ameshindwa tekeleza ahadi yake
juu ya mwanamke huyu? HAIWEZEKANI, kwani imeandikwa Mungu ni muweza wa yote (Mathayo 19:26, Luka 1:37, Marko 10:27 ), pia
imeandikwa Bwana hakawii kutimiza ahadi
yake (2 Petro 3:9), na pengine tunakiri Mungu si binadamu kubadilisha mawazo yake (1 Samueli 15:29 )
Tunaelewaje kuhusu Utakaso wa Maria katika Hekalu la Bwana(Luka
2:22), Je mstari huu haupingani na fundisho hili?
“Siku
zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Musa,
wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya
Bwana”
Mstari
huu unazungumzia Maria aliyehitaji kutakaswa Hekaluni baada ya kumzaa mtoto Yesu.
Hii ilikua ni sheria ya Torati ya Musa iliyohitaji kila mwanamke baada ya
kujifungua, inampasa kujitokeza mbele ya Hekalu la Bwana na kutoa sadaka ili
apate kusafishwa dhambi ya uchafu uliotokana na kujifungua. Kama Maria alikua
msafi asiye na doa la dhambi mbona ilimpasa pia yeye kusafishwa? Hapa jibu
linalotolewa ni sawa na jibu alilotoa Kristu kwa Yohana Mbatizaji wakati Yesu
anakuja kubatizwa naye. Ubatizo wa Yohana ulikua ni wa Toba na wa kuondolewa
dhambi na kusafishwa. Lakini Yesu asiye na doa la dhambi hakuhitaji ubatizo
huo. Pia hakuja kutengua sheria ya Torati, hivyo ili haki itendeke anamwambia
Yohana “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana
kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka” (Mathayo 3:15).
Ni hivyo hivyo ilivyotendeka kwa Maria alipohitaji kusafishwa kutokana na sheria
za Torati. Si kusafishwa kwa ajili ya dhambi maana hakua na hata moja. Bali
alikubali na kuheshimu sheria ili “haki yote itendeke”
Maria Sanduku Jipya la Agano
Katika kitabu cha agano la kale, kama
jinsi Mungu alivopendelea kukaa ndani ya Sanduku la Agano ambalo lilikua
takatifu na lenye usafi, vivyo hivyo alipendelea kushuka duniani na kukaa miezi
tisa ndani mwa sanduku jipya la agano lililo safi yaani Mama Maria. Hivyo basi
ndio maana Kanisa hadi hivi leo kupitia mafundisho ya mababa wa Kanisa na
mapokeo ya mitume, Mama Maria anaitwa Sanduku jipya la Agano maana Mungu alikaa
tumboni mwake kwa miezi tisa. Mt Luka katika injili yake anatupatia uhusiano
huo kwa kuonyesha furaha aliyopata Yohana mbatizaji akiwa tumboni mwa mamaye
Elizabeth wakati Maria amekwenda mtembelea. Elizabeth anasema mtoto Yahona
alicheza kwa furaha. Vivyo hivo Mfalme Daudi pia alicheza kwa furaha mara tu
baada ya kurudishwa Sanduku la agano ambapo ndani yupo Mungu (2 Samueli 6:14)).
Elizabeth bila hata kujua habari alizopashwa Maria, anajazwa na Roho Mtakatifu
na kumlaki Maria kama Mama wa Bwana ambaye ni Mungu mwenyewe katika nafsi ya
pili
Mwisho kabisa Mama Maria mwenyewe amedhihirisha ukweli wa fundisho hili kwetu.
Kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, Kanisa huadhimisha sikukuu ya Mama yetu
wa Lourdes ambapo tunakumbuka Mama Maria kumtokea Mt Benardetta na
kujitambulisha jina kama "Ni mimi niliye kingiwa dhambi ya asili "
peleka ujumbe wangu kwa wote kwamba watubu na kusali na kumwamini Yesu Kristu
ili waokoke. Maria alimtokea kwa mara ya kwanza Mt. Benardeta mwaka 1858 huko Loudes
ufaransa
Je, aheshimike Milele?
Anayekubali mafundisho haya ndiye
mshika neno la Mungu katika uhalisia wake. Neno la Mungu linatusihi kumheshimu
Mama daima katika vizazi vyote vya kale na vijavyo. Biblia inatuambia kuwa
tangu kutungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, inatupasa watu wote kumwita
Mama Maria “Mwenye Heri”. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri (Luka
1:48). Biblia kutumia neno “Tangu
sasa” inataka kutuonyesha kuwa heshima anayopata Mama Maria hadi hivi leo si
ngeni kama ilivyoanza kukataliwa na wakristu wenzetu karne ya 16. Heshima hiyo
alipewa “Tangu” kipindi kile cha Kristu. Biblia ya Kiingereza inatumia maneno “All generations will call me blessed”. Maneno
“All generations” ikimaanisha kila kizazi cha binadamu toka kipindi cha Kristu,
kipindi cha matendo ya Mitume, kipindi tunachoishi kwa sasa na daima kitamheshimu
Mama wa Mungu na kumwomba atuombee kwa mwanaye Kristu Mfalme ili tupate wokovu
Maria Mama wa Mungu, utuombee sasa na wakati wa kufa kwetu. AMINA