Leo Kanisa limeanza
kipindi cha Kwaresima. Hizi ni siku arobaini za sala, mafungo, kujinyima,
kutubu na kuwasaidia wahitaji. Ni kipindi cha maandalizi ya sikukuu ya Ufufuko
wa Yesu. Neno linalotuongoza ni wongofu.
Kwaresima ni safari inayomrudisha mkristo kwenye njia ya wongofu: nirudieni mimi! Hivyo ndivyo Bwana
anavyotuhimiza. Anataka tumrudie, si kwa matendo ya nje, bali kwa mioyo yetu yote kwa kurarua mioyo na si mavazi.
Mafungo ya Kwaresima
si ya kujikatalia kula tu, bali pia kuacha kabisa mawazo, maneno na matendo
yanayopunguza mwendo wetu wa safari ya kiroho. Ni kipindi cha ibada ya moyo na
cha kutenda matendo ya huruma yanayoonesha mshikamano wa kibinadamu na upendo
wa kikristo unaookoa. Kama anavyosema Mt. Petro Krisologo; “Matendo ya huruma
na ibada ndiyo mabawa ya mfungo… mfungo bila matendo ya huruma ni sanamu ya
njaa, ni muonekano wa nje usio na thamani ya utakatifu. Bila ibada mfungo ni
fursa ya ubinafsi… tunapofunga, ndugu zangu, tuweke chakula chetu mikononi mwa
maskini” (Petro Krisologo, Omelia VIII,
Sul digiuno della Quinquagesima)
Kipindi hiki
kinapaswa kuwa kipindi kinachotusaidia kuanza tukio la kinabii, tukio
linalosaidia kuyabadili maisha yetu na ya wenzetu. Katika Biblia Musa anafunga
siku arobaini usiku na mchana kabla ya kupokea Amri Kumi za Mungu (Rej. Kut 34:28),
anafanya hivyo pia Elia kabla hajakutana na Mungu juu yam lima Horebu (1Fal
19:8), hali kadhalika Yesu kabla hajaanza utume wake.
Kipindi
cha Kwaresima kinaanza siku ya Jumatano ya Majivu. Don Tonino Bello, aliyekuwa
Askofu wa Molfetta, Italia anaandika kuwa safari yote ya mkristo ni kuanzia
kichwani hadi miguuni. Ni safari inayoelezwa vizuri kwa ishara ya majivu
tunayopakwa kichwani na maji anayotumia Yesu kuwaosha mitume wake miguu. Ni
safari inayoanzia kwenye toba na kuishia kwenye utumishi. “Toba na utumishi”,
anasema Don Tonino Bello, “ni mahubiri makuu ambayo kanisa linayakabidhi kwa
majivu na maji, kuliko kwa maneno”. Kwa maneno mengine ndiyo kusema kuwa
mahubiri yetu hayawezi kuielezea vizuri zaidi safari ya uongofu kama jinsi
ambavyo ishara ya majivu na maji inavyoweza kufanya. Tumrudie Mungu kwa moyo wa
toba na katika utumishi tuzidi kuiona ile sura ya Mungu katika mahujaji wote
walio katika safari ya maisha.