Katika waraka wake wa Kitume Porta
Fidei (Mlango wa Imani) wa
tarehe 11 Oktoba 2011, Baba
Mtakatifu Benedikto XVI alitangaza Mwaka wa Imani ulioanza tarehe 11 Oktoba
2012 na utakaofikia kilele chake tarehe 24 Novemba 2013. Katika hati hiyo, Baba
Mtakatifu anawaalika Wakatoliki wote duniani kurudia upya imani yao kwa Baba,
kwa Mwana na kwa Roho Mtakatifu na kurudia upya imani yao katika mafundisho ya
msingi ya Kanisa. Mwaka wa Imani unaadhimisha pia matukio matatu ya kihistoria:
- Tukio la kwanza ni kumbukumbu ya miaka 50 tangu ulipoanza rasmi Mtaguso wa pili wa Vatikano (11 Oktoba 1962).
Huo uliitishwa na Baba Mtakatifu Yohane XXIII na uliwajumuisha maaskofu wote wa
Kanisa Katoliki. Mtaguso ulianza mwaka 1962 na kufungwa mwaka 1965 ukitoa hati
16 za Mtaguso zilizotoa mwongozo wa kichungaji juu ya masuala mbalimbali
yanayohusu Kanisa na jamii. Moja ya
malengo ya Mwaka wa Imani ni “kusoma kwa ufasaha” hati za Mtaguso na “zizingatiwe kuwa matini muhimu za kisheria”
za mamlakafunzi ya Kanisa (Porta Fidei,
5).
- Tukio la pili ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu ilipochapwa rasmi Katekisimu ya Kanisa Katoliki (11 Oktoba 1992).
Mwaka wa Imani ni fursa ya kuwasaidia
Wakatoliki “kuvumbua upya na kujifunza msingi wa mafundisho ya imani unayopata muhtasari wake ulionyambuliwa na wa
kimantiki katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki (Porta Fidei, 11).
- Tukio la tatu ni Sinodi ya kawaida ya Maaskofu juu ya uinjilishaji Mpya, ambayo ilifanyika Roma tarehe 7-28 Oktoba 2012.
Mada ya Sinodi
hiyo ilikuwa ni “Uinjilishaji Mpya kwa
ajili ya kueneza imani ya kikristo”.
Baba Mtakatifu anapenda Mwaka wa Imani uwasaidie wakristo “kutangaza
neno la ukweli ambalo Bwana alituachia” (Porta
Fidei, 6) kwa sababu “upendo wa Kristo unatubidisha ... kuinjilisha” (Porta Fidei, 7). Pia “Imani inakuwa pale
inapotiwa katika maisha kama uzoefu wa upendo ilipokelewa na pala
inaposhirikishwa kwa wengine kama uzoefu wa neema na furaha” (Porta Fidei, 7).